Tulitumia kinga! Eric Omondi 'aruka' mtoto wa Maribe, adai thibitisho kuwa ndiye baba mzazi kabla akubali kuwajibika

Muhtasari

•Omondi alidai kwamba alishiriki tendo la ndoa na Maribe mara moja tu mnamo mwaka wa 2012 baada yao kubugia chupa kadhaa za mvinyo. 

•Amesema kwamba alishtuka sana wakati Bi. Maribe alimpigia simu miezi miwili baadae akimweleza kuwa alikuwa amebeba ujauzito wake ilhali kinga ilitumika wakati walipokuwa wanashiriki mchezo wa kitandani.

•Amesema kwamba atakubali kusaidia katika malezi ya mvulana huyo wa miaka saba iwapo tu Maribe atakubali wafanye vipimo vya DNA.

Image: HISANI

Mcheshi mashuhuri nchini Eric Omondi sasa anatilia shaka kuwa ndiye baba mtoto  wa mtangazaji Jackie Maribe.

Usiku wa Jumanne Omondi alitumia ukurasa wake wa Instagram kueleza kwamba hakuwahi kuwa kwenye mahusiano na Maribe bali kwa wakati alikuwa anachumbia mtangazaji mwingine.

Omondi alidai kwamba alishiriki tendo la ndoa na Maribe mara moja tu mnamo mwaka wa 2012 baada yao kubugia chupa kadhaa za mvinyo. 

"Tulipatana Radio Africa mwaka wa 2012. Nilikuwa nafanya kazi Radio Jambo na Jacque alikuwa anafanya kazi Kiss TV. Usiku mmoja baada ya sherehe na kunywa chupa kadhaa za whiskey na mvinyo Jacque na mimi ikatendeka. Ilikuwa jambo la usiku mmoja kwani alikuwa anachumbia Sam Ogina wa KTN" Omondi alisema. 

Mchekeshaji huyo asiyepungukiwa na drama amedai kwamba alihakikisha kwamba ametumia kinga wakati aliposhiriki mapenzi na Maribe.

Amesema kwamba alishtuka sana wakati Bi. Maribe alimpigia simu miezi miwili baadae akimweleza kuwa alikuwa amebeba ujauzito wake ilhali kinga ilitumika wakati walipokuwa wanashiriki mchezo wa kitandani.

"Tulitumia kinga!!  Baada ya miezi miwili Jacque aliniambia kuwa ni mjamzito!! Mara moja nilimuuliza ikawaje ilhali tulitumia kinga?? Aliniambia kuwa hiyo haijalishi kwani mama ndiye hujua baba mzazi wa mtoto wake" Alidai Omondi.

Omondi ameweka wazi kwamba hakuwahi shiriki tendo la kitandani tena na mtangazaji huyo kwa kipindi ambacho alikuwa mjamzito  na kudai kuwa walionana mara moja moja tu.

Mchekeshaji huyo amedai kuwa baada ya mtoto kuzaliwa aliagiza Maribe wafanye vipimo vya uzazi (DNA) ili athibitishe kuwa ndiye baba ya mtoto yule ila mtangazaji yule hakukubaliana na agizo lake.

"Takriban miezi minne baada ya mtoto kuzaliwa Jacque alinipigia simu akaniulia kama nitamsaidia kulea  ama nitakuwa maishani ya mtoto yule. Niliomba tufanye DNA ili nikubali kuwa maishani ya mtoto na nimsaidie kulea.  Alikasirika na akakataa ombi langu. Kwa miaka saba nimebembeleza Jacque akubali tufanye vipimo vya DNA lakini ameendelea kukataa!!" Alisema Omondi.

Amesema kwamba atakubali kusaidia katika malezi ya mvulana huyo wa miaka saba iwapo tu Maribe atakubali wafanye vipimo vya DNA.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya Maribe kumushtumu Omondi kuwa baba asiyewajibikia mtoto wake. 

Maribe alidai kwamba kwa miaka saba ambayo imepita amegharamia mahitaji yote ya mwanawe pekee yake bila usaidizi wowote wa Omondi.