Ndoa na gavana Mutua? Lilian Ng'ang'a asema walikuwa washirika wa muda mrefu tu

Muhtasari

•Mpenzi huyo wa sasa wa mwanamuziki Juliani ameweka wazi kwamba uhusiano wake na gavana Mutua ulikuwa ushirikiano wa muda mrefu.

•Lilian amesema kwamba hapajakuwa na uhusiano mzuri kati yake na Mutua tangu kutengana kwao, tofauti na madai ya gavana huyo kwenye mitandao ya kijamii.

•Lilian amedai kwamba gavana Mutua amekataa kabisa kusonga mbele na maisha yake licha ya mahusiano yao kufika kikomo mapema mwaka huu.

Image: INSTAGRAM//GOVERNOR ALFRED MUTUA

Bi Lilian Ng'ang'a amepuuzilia mbali ndoa yake na gavana wa Machakos Alfred Mutua.

Alipokuwa anahutubia wanabari siku ya Jumatano, Lilian amesema kwamba hakuwa ameolewa kihalali na mwanasiasa huyo.

Mpenzi huyo wa sasa wa mwanamuziki Juliani ameweka wazi kwamba uhusiano wake na gavana Mutua ulikuwa ushirikiano wa muda mrefu.

"Hatukuwa tumefunga ndoa kisheria. Tulikuwa washirika wa miaka mingi" Lilian alisema.

Wawili hao walitangaza kutengana kwao mnamo mwezi Agosti ingawa walikuwa wamekosana miezi miwili kabla ya kufichua hadharani.

Lilian amesema kwamba hapajakuwa na uhusiano mzuri kati yake na Mutua tangu kutengana kwao, tofauti na madai ya gavana huyo kwenye mitandao ya kijamii.

"Nilitamatisha uhusiano wangu na Alfred Mutua mwezi Juni mwakani. Mara kadhaa haswa wiki katika kipindi cha wiki mbili zilizopita  nimeona Mutua akisema kwa gazeti na mitandaoni kuwa sisi ni marafiki na eti uhusiano wetu ulitamatika kufuatia maafikiano ya pamoja. Huo ni uongo wake wa kawaida. Hatujazungumza naye tangu mwishoni mwa mwezi Agosti. Lilian amesema.

Lilian amedai kwamba gavana Mutua amekataa kabisa kusonga mbele na maisha yake licha ya mahusiano yao kufika kikomo mapema mwaka huu.

Walipokuwa wanatangaza kutengana kwao mwezi Agosti, gavana Mutua aliahidi kuwa wangeendelea kuwa marafiki wazuri na kudai kuwa angeendelea kuomba Lilian ushauri.

Hata hivyo Lilian amesema kwamba Mutua aliathiriwa sana na kutengana huku na kufuatia hayo amekuwa akimpa vitisho pamoja na walio karibu naye.

Bwana Mutua ameguswa sana na kutengana kwetu. Ingawa nilisema nataka kusonga mbele na maisha yangu, alifikiria vingine" Lilian amesema.

Lilian amesema kwamba mgombeaji huyo wa kiti cha urais mwaka ujao anatazamia kuchukua kila kitu anachomiliki huku tayari akiwa amemwagiza arejeshe  pesa zote ambazo aliwahi kumpatia ama kutumia juu yake.