"Tumekuwa na vita zetu kisiri" Eric Omondi afunguka kuhusu uhusiano wake na Jackie Maribe

Muhtasari

•Omondi amesema kwamba hatua ya kufanya vipimo vya DNA imekuwa suala la vuta nikuvute kati yake na Maribe kwa muda mrefu.

•Omondi amekiri kwamba amewahi jaribu kufanya vipimo vya DNA kwa kutumia nywele za mtoto anayedaiwa kuwa wake bila idhini ya Maribe ila akaambiwa haiwezekani bila kuwepo kwa mama.

Image: HISANI

Mchekeshaji Eric Omondi amesema kuwa hajaanza sasa kusisitiza kuthibitisha iwapo ndiye baba mzazi wa mwanawe Jackie Maribu.

Omondi amesema kwamba hatua ya kufanya vipimo vya DNA imekuwa suala la vuta nikuvute kati yake na Maribe kwa muda mrefu.

Alipokuwa kwenye mahijiano na Massawe Japanni katika kitengo cha 'Ilikuwaje', mchekeshaji huyo  alidai kwamba amekuwa akisihi Maribe wafanyie mtoto vipimo vya DNA tangu alipozaliwa miaka saba iliyopita.

"Sijadai vipimo vya DNA miaka saba baadaye, nimekuwa nikimuomba tupimwe kwa kipindi cha miaka saba" Omondi alisema.

Amesema kuwa licha ya kwamba amekuwa akisisitiza kuhusu suala la DNA kwa miaka mingi, bi. Maribe amekuwa akipinga ombi lake kila wakati.

Omondi amekiri kwamba amewahi jaribu kufanya vipimo vya DNA kwa kutumia nywele za mtoto anayedaiwa kuwa wake bila idhini ya Maribe ila akaambiwa haiwezekani bila kuwepo kwa mama.

"Nimejaribu mara kadhaa. Niko na nywele za mtoto kwa nyumba yangu, ni halali. Nilienda Aghakhan. Siwezi fanya vipimo hivyo bila kuwepo kwa mama mzazi" Omondi alisema.

Mchekeshaji huyo alifichua kwamba wamekuwa wakilumbana na Maribe kisiri kwa muda mrefu ila hawakuwahi onyesha mzozo wao hadharani hapo awali.

Omondi ameapa kwamba kamwe hajawahi kataa mtoto huyo.

"Tumekuwa na vita zetu kisiri ambazo hatujawahi ambia Wakenya. Mimi sijawahi kataa mtoto. Mimi na Jackie tumekuwa na vita zetu. Nimekuwa nikimwambia DNA anakataa. Ili tusiweke mtoto faraghani tumekuwa  tumenyamazia" Alisema Omondi.

Omondi amemnyooshea Maribe kidole cha lawama kufuatia drama ambazo zimekuwepo kati yao hivi karibuni.

Amesema kwamba aliamua kuweka suala la DNA hadharani kufuatia madai ya Maribe kwamba hajakuwa baba mwajibikaji tangu mtoto azaliwe.

Hata hivyo Omondi amekiri kwamba ni kweli hajahusika sana katika ulezi wa mtoto kwa sababu bado anashuku huenda si yeye baba mtoto.

"Sipo. Nipo maishani ya mtoto kidogo kidogo nataka niwe kikamilifu. Natekeleza majukumu madogo sana. Ata karo ya shule sijalipa. Naenda naona mtoto, namnunulia simu, naenda graduation, namnunulia vitu kidogo. Tulikubaliana kwamba iwapo anataka niwajibikie mtoto tufanye vipimo vya DNA" Omondi.

Omondi alisema kwamba haikuwa nia yake kuweka mtoto hatarini ya kudhihakiwa na kutusiwa mitandaoni.