'Endelea na maisha yako kwa amani utapona!' Sonko ashauri Mutua kufuatia madai kwamba amekuwa akitishia Lilian Ng'ang'a

Muhtasari

•Gavana huyo wa zamani amedai kwamba pia yeye amekuwa akizozana na mwanadada  fulani ila akaeleza kuwa hajapiga hatua ya kudai kurejeshewa  mali yake kama Mutua anavyodaiwa kufanya.

Gavana Alfred Mutua, Mike Sonko
Gavana Alfred Mutua, Mike Sonko
Image: HISANI

Gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari siku ya Alhamisi ilikuwa kuhusu  malalamishi ya Lilian Ng'ang'a dhidi ya aliyekuwa mpenzi wake gavana Alfred Mutua.

Lilian ambaye kwa sasa anachumbia mwanamuziki Julius Owino almaarufu kama Juliani alidai kwamba gavana Mutua amekataa kabisa kusonga mbele na maisha yake licha ya mahusiano yao kufika kikomo mnamo mwezi Juni mwakani.

Alisema kwamba  hatua ya kutamatika kwa uhusiano wao iliathiri gavana Mutua sana na kutokana na hayo amekuwa akimhangaisha na kumpa vitisho pamoja na walio karibu naye.

"Bwana Mutua ameguswa sana na kutengana kwetu. Ingawa nilisema nataka kusonga mbele na maisha yangu, alifikiria vingine" Lilian amesema

Lilian alidai kwamba Mutua alimtishia kuwa tayari kuna watu ambao wamejipanga kumuangamiza pamoja na marafiki wake.

"Alisema kuwa kuna watu wamejitolea kuua watu walio karibu nami na akatishia kuwa huenda akakubali  ili apatie baadhi yao funzo. Kwa dharau alisema kuwa yeye ni mtu wa maana sana nchini na anaweza fanya chochote alichokuwa amepanga kunifanyia pamoja na marafiki wangu na asiadhibiwe. Alisema kuwa kuna watu ambao wako tayari na wamesubiri kunimaliza pamoja na marafiki wangu" Lilian amesema.

Kama kawaida aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko huwa hachelewi kutoa mchango wake kwenye mdahalo wowote unaoenea nchini kwa wakati.

Sonko amejitokeza kumshauri mwanasiasa mwenzake akubali kusahau yaliyopita na aangazie kuponya maumivu ya moyo wake.

Gavana huyo wa zamani amedai kwamba pia yeye amekuwa akizozana na mwanadada  fulani ila akaeleza kuwa hajapiga hatua ya kudai kurejeshewa  mali yake kama Mutua anavyodaiwa kufanya.

"Huu unakaa kuwa msimu wa utengano. Lakini mapenzi kwa wakati mwingine yaweza kuumiza. Kutoka kwa yaliyotendekea Agnes Tirop na sasa Lilian na Kavakulu. Hata mimi kuna dame ameniletea ufala lakini nimemwachia hadi kila kitu ya nyumba. Kavakulu songa mbele kwa  amani utapona!" Sonko amesema.

Alipokuwa anahutubia wanahabari siku ya Alhamisi, Lilian alidai kwamba mgombeaji huyo wa kiti cha urais mwaka ujao anatazamia kuchukua kila kitu anachomiliki huku tayari akiwa amemwagiza arejeshe  pesa zote ambazo aliwahi kumpatia ama kutumia juu yake.

"Nilimuomba tumwe na utengano mzuri na nikamkumbusha kwamba hatukuwa tumefunga ndoa. Mutua aliniita adui nambari moja, alitishia 'kunivunja niwe jivu' akichukua kila kitu nilicho nacho na ninachomiliki. Kusema kweli tayrai ameanza kwani ameambia mawakili wake waagize pesa zote ambazo amewahi kunipatia ama kuidhinisha itumike juu yangu" Lilian amesema.

Ameweka wazi kwamba  hakuwa mke wala mpenzi wa Mutua ila walikuwa washirika wa muda mrefu tu.