"Siwezi kufanya hivi tena, Tuwache tu!" Jackie Maribe aomba Wakenya wampe amani sasa

Muhtasari

•Maribe ametumia ukurasa wake wa Instagram kusihi Wakenya wamuache sasa kuona kuwa amekuwa mada kwa siku kadhaa sasa.

•Maribe amesihi Wakenya wajali na kuheshimu mtoto asiye na hatia ambaye anahusika katika mzozo wake na Omondi

Image: INSTAGRAM// JACKIE MARIBE

Huku jina lake likiendelea kuvuma kwenye vyombo vya habari na mitandaoni kufuatia drama zilizojitokeza hivi karibuni, Jackie Maribe sasa amejitokeza kutoa ombi muhimu kwa Wakenya.

Mwanahabari huyo wa zamani ambaye amekuwa akiangaziwa sana mitandaoni pamoja na mcheshi Eric Omondi ametumia ukurasa wake wa Instagram kusihi Wakenya wamuache sasa kuona kuwa amekuwa mada kwa siku kadhaa sasa.

Maribe amesihi Wakenya wajali na kuheshimu mtoto asiye na hatia ambaye anahusika katika mzozo wake na Omondi

"Hii ni taarifa yangu ya mwisho kuhusiana na hadithi hii ambayo haiishi. Nataka kuachwa pekee  yangu. Huenda tulifanya zaidi. Huenda tulidiwa nguvu. Kila mmoja wetu atamiliki ukweli wetu. Kuna mtoto anayehusika kwa hivyo naomba tumheshimu. Siwezi kufanya hivi tena" Maribe amesema.

Haya yanajiri siku moja tu baada yake na Omondi kuomba msamaha kufuatia matendo yao yenye aibu kwenye mitandao ya kijamii.

Wawili hao waliletwa pamoja na mjasiriamali mashuhuri Simon Kabu siku ya Alhamisi na wakawa na maafikiano mazuri.

Maribe na Omondi walikiri kwamba walifanya kosa kubwa kuvuruta mtoto kwenye ugomvi wao na kumuweka kwenye faragha.

"Mimi na Jackie tumepelekana. Tunaomba msamaha. Tulikosea" Eric Omondi alisema.

Video ya wawili hao wakiwa  wamekumbatiana vizuri  huku wakisikiza ushauri kutoka wa Kabu imekuwa ikisambazwa sana mitandaoni.