'Chochote kikinitendekea na Juliani, Alfred Mutua ndiye mhusika!' Lilian Ng'ang'a asisitiza maisha yake yamo hatarani

Muhtasari

•Lilian amesema kwamba kwa kipindi cha miezi mitatu ambayo imepita amekuwa akiomba gavana huyo wa Machakos wawe na utengano wa amani ila juhudi zake hazijaweza kufua dafu.

•Lilian amewashauri wauaji ambao wamelipwa kumuangamiza pamoja na mpenziwe wasikubali kutumiwa katika mzozo ambao hawahusiki.

Aliyekuwa mpenzi wa gavana Mutua Lilian Ng'ang'a
Aliyekuwa mpenzi wa gavana Mutua Lilian Ng'ang'a
Image: MERCY MUMO

Siku chache tu baada ya kuvunja kimya kuhusu vitisho ambavyo amekuwa akipatiwa na aliyekuwa mpenzi wake gavana Alfred Mutua, Lilian Ng'ang'a ameendelea kusisitiza kwamba maisha yake yamo hatarini.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Lilian amesema kwamba kwa kipindi cha miezi mitatu ambayo imepita amekuwa akiomba gavana huyo wa Machakos wawe na utengano wa amani ila juhudi zake hazijaweza kufua dafu.

Lilian amesema hapo awali alikuwa amechagua kusalia kimya kuhusu yote ambayo yamekuwa yakiendelea ila sasa ameonelea heri ayafichue hadharani kuona kwamba Mutua amekuwa akichukua fursa ya ukimya wake.

"Siku zote nimeishi kupendelea  na bado napendelea maisha ya utulivu. Kwa kuwa Alfred anajua sipendi vyombo vya habari, alichagua kupigana nami na kunikosesha amani hadharani akijua sitazungumza. Amekuwa akienda kwenye vyombo vya habari akidai kuwa sisi ni marafiki, bila aibu. Yale yote ambayo nimefichua sasa yamekuwa yakiendelea tangu Agosti. Nimekuwa kimya na nimekuwa nikimuomba tutengane kwa amani" Lilian amesema.

Mpenzi huyo wa Juliani wa sasa amesisitiza maisha yake na ya mpenziwe yamo hatarini huku akionya kuwa iwapo chochote kitawafanyikia basi Mutua ndiye  atakakuwa amehusika.

Lilian amewashauri wauaji ambao wamelipwa kumuangamiza pamoja na mpenziwe wasikubali kutumiwa katika mzozo ambao hawahusiki.

"Kitu chochote kikitendekea Juliani na mimi, Alfred Mutua ndiye mhusika. Wale ambao wamelipwa kutuua wawe na hekima na wajiulize kama Alfred anaweza kufanya kazi zao chafu kama majukumu yanaweza badilishwa. Hakuna yeyote anayefaa kutumiwa katika mizozo ambayo hawajui chochote kuhusu kwa sababu ya pesa kidogo" Lilian amesema.

Pia ameshauri wanaoendesha mitandao ya kijamii ya Mutua dhidi ya kukubali kutumiwa vibaya katika vita za kibinafsi za gavana huyo

"Aibu kwenu nyote!! Nawashauri mzingatie kumfannya awe rais. Anaweza kuwa rais mzuri!" Amesema Lilian.