"Tangu muoe mambo hayajakuwa sawa!" Eric Omondi ashambulia wanamuziki Sauti Sol, Khaligraph, Bahati

Muhtasari

•Mcheshi huyo asiyepungukiwa na utata maishani ametoa wito kwa wanamuziki wa Kenya watie bidii zaidi kazini huku akidai kuwa sekta ya burudani hapa nchini imekufa.

•Omondi amedai kuwa bendi ya Sauti Sol, rapa Khalighraph Jones na mwanamuziki aliyegura injili Bahati pekee ndio tumaini ya sekta ya burudani nchini

Image: INSTAGRAM

Siku chache tu baada ya kutumbuiza na drama kochokocho pamoja na 'baby mama' wake Jackie Maribe, Eric Omondi sasa ameamua kuingilia wanamuziki wa Kenya.

Mcheshi huyo asiyepungukiwa na utata maishani ametumia ukurasa wake wa Instagram kutoa wito kwa wanamuziki wa Kenya watie bidii zaidi kazini huku akidai kuwa sekta ya burudani hapa nchini imekufa.

Omondi amewashinikiza wasanii waamke huku akidai kuwa wengi wao wameisha, wamezembea  na wanachosha.

"Tumekuwa wa kutohitajika, wa kutabirika na wa kuchosha. Tunahitaji kutia bidiii zaidi ili turudishe utukufu uliopotea. Lazima tuwekeze kwa sanaa. Mungu anajua mimi najaribu kadri  niwezavyo" Omondi amesema.

Omondi amedai kuwa bendi ya Sauti Sol, rapa Khalighraph Jones na mwanamuziki aliyegura injili Bahati pekee ndio tumaini ya sekta ya burudani nchini.

Hata hivyo amesema kwamba ubabe wao katika sanaa umekuwa ukididimia tangu walipopiga hatua ya kufunga ndoa.

"Hatua ya kwanza ya kutatua tatizo lolote ni kukubali kwamba tasnia yetu ya muziki haijawa sawa. Ujumbe wangu ni kuwa tulipoteza kitu na wazo langu ni pamoja tunaweza kuitafuta na kuirudisha. @sautisol @khaligraph_jones na  @bahatikenya nyinyi ndio tumaini letu lakini ukweli usemwe, tangu muoe mambo hayajakaa sawa😥😥😥. Siwezi kukaa na kutazama sekta yetu ya muziki ikilala na kunyamaza kabisa, Lazima tu nifungue roho. @sautisol najua tuko peke pamoja na tunashukuru kila wimbo mmetoa kibinafsi lakini kikundi kikinyamaza ni sekta na mashabiki ndio wanaumia. Hata sijui kwanini nawabembeleza. AMKENI BWANAAA!!! AMKENIIIII MUMELALAAA na huo ndio UKWELI MKUBWA!!!! @bienaimesol wewe Nunua WIG kwanza ufunike KIPARA kabla ya uongeleshe  rais. Shenzi" Omondi amesema.

Wanamitandao wengi ikiwemo wasanii kadhaa kama Jua Cali, Khaligraph, Bien, Femi One na Svara wamejitokeza kukosoa maneno ya Omondi.