"Eric ni muongo!" Monica Ayen ataja sababu zilizomsukuma kukatiza uhusiano wake na Eric Omondi

Muhtasari

•Ayen alisema kwa kipindi kifupi ambacho wamekuwa pamoja, Omondi amemdanganya  kuhusu mambo mengi yasiyohesabika.

•Malkia huyo kutoka Sudan Kusini alisema Omondi alimfanya akiuke mila nyingi za jamii yake ila kama punda tu shukran zake zimekuwa mateke.

•Alisema jambo lililomkera zaidi hadi akapoteza matumaini na ndoa yao ni drama iliyojitokeza kati ya Omondi na baby mama wake Jackie Maribe.

Eric Omondi na Monica Ayen
Eric Omondi na Monica Ayen
Image: INSTAGRAM

Mshindi wa Wife Material 3, Monica Ayen ameeleza ziadi kuhusu utengano wake na mchekeshaji Eric Omondi.

 Alipokuwa kwenye mahojiano na Mungai Eve masaa machache baada ya kutangaza uamuzi wake wa kumtema  Omondi, Ayen alimshtumu mchekeshaji huyo kuwa muongo kupindukia huku akisema alishindwa kuuvumilia uwongo wake tena.

Ayen alisema kwa kipindi kifupi ambacho wamekuwa pamoja, Omondi amemdanganya  kuhusu mambo mengi yasiyohesabika.

"Eric ni muongo. Amedanganya kuhusu mambo mengi. Mara ngapi nimemuuliza ataenda kuona wazazi wangu lini? Alikuwa ameniahidi tungeenda kuona wazazi Jumapili kwa kuwa ni siku ya sabato ila  ilipofika akaniambia amesahau. Utawezaje kusahua uko na mtu kwa nyumba na mnafaa kuenda kuona wazazi wake. Mimi siwezi kuvumilia" Ayen alisema.

Malkia huyo kutoka Sudan Kusini alisema Omondi alimfanya akiuke mila nyingi za jamii yangu ila kama punda tu shukran zake zimekuwa mateke.

"Mwanzo ata hufai kuwa na mwanaume kabla hajaenda kuona wazazi. Hata sikumtambulisha kwa wazazi mwanzoni na hilo ni jambo mbaya. Nilijiunga na Wife Material kwa sababu alisisitiza nije. Nahisi nilivunja mila ila hata haonyeshi shukran. Inaumiza moyo" Ayen alisema.

Ayen alisema ingawa alifahamu mchekeshaji huyo anapenda wanawake matarajio yake yalikuwa kwamba angemuonyesha heshima.

Alisema jambo lililomkera zaidi hadi akapoteza matumaini na ndoa yao ni drama iliyojitokeza kati ya Omondi na baby mama wake Jackie Maribe.

Ayen alieleza kwamba Omondi hakuwahi mfichulia kuwa yeye ni baba licha ya kuwa hapo awali alikuwa amemuuliza iwapo ana mke na watoto.

"Drama zake na baby mama zilinikera zaidi. Mwanzo hata hakuniambia ana mtoto. Nilimuuliza mara nyingi, tukiwa kwa shoo tulikuwa tunazungumza. Nilimuuliza ikiwa ana mke na watoto akasema hapana, eti angali mdogo kuwa na familia. Nilishuka kuona baby mama akizungumza kuhusu baba asiyewajibika. Aliniomba msamaha huku akidai kuwa alikuwa anajipanga kuniambia" Alisema.

Ayen alisema wakati drama zile zilikuwa zinaendelea alimshauri Omondi aache kujibizana na Maribe mitandaoni kwani kitendo kile hakikuwa kizuri.

Alisema kuwa ujauzito bandia ambao Omondi alidai kampachika Miss P haukumpa wasiwasi kwani tayari mchekeshaji huyo alikuwa amemweleza kuwa ni kiki tu walikuwa wanatafuta.

Ingawa aliapa hawezi kurudiana na mchekeshaji huyo, Ayen alisema hakufurahia kutengana kwao.