"Zuuh ni mpenzi wangu wa kwanza" Harmonize akiri mapenzi makubwa kwa bintiye na kufichua utata uliozingira kuzaliwa kwake

Muhtasari

•Konde Boy alifichua kwamba mwanadada huyo alikuwa na wasiwasi kuhusu ujauzito huo na hata alikuwa tayari kuutoa ila mwanamuziki huyo akamkataza.

•Alifichua utata mwingi ulizuka kuhusiana na uzazi wa malkia yule hadi akalazimika kufanya vipimo vya DNA baada ya kupata fununu kuwa huenda sio yeye baba mzazi.

•Harmonize amemuomba binti yake msamaha katika kibao chake cha kwanza kwenye albamu yake mpya.

Image: INSTAGRAM// HARMONIZE

Nyota wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarufu kama Harmonize amefunguka kuhusu utata uliozingira kuzaliwa kwa binti yake Zulekha Nasra.

Alipokuwa anafafanulia mashabiki wake maana ya nyimbo zilizo kwenye albamu yake ya pili 'High School' hivi  majuzi, mwanamuziki huyo alifichua kwamba kuzaliwa kwa mtoto huyo ndicho chanzo cha kuvunjika kwa ndoa yake ya kwanza na Sarah Michelloti.

Harmonize alisema ndoa yao ya miaka minne ilianza kusambaratika wakati mpenzi wake alikuwa amesafiri kuenda kwao na baada ya kuwa pweke kwa muda akapata majaribu ya kutembea na mwanadada aliyemzalia mtoto.

"Ilikuja kipindi akawa anasafiri kuenda kwao. Nilikuwa Tanzania na kama unavyojua umbali wa mapenzi unapokuwa nikaishia kutembea na mwanamke ni mama Zuuh sasa hivi. Kwa mipango ya mwenyezi Mungu nikamfanya mjamzito." Harmonize alisema.

Konde Boy alifichua kwamba mwanadada huyo alikuwa na wasiwasi kuhusu ujauzito huo na hata alikuwa tayari kuutoa ila mwanamuziki huyo akamkataza.

Alisema kuwa alikubali majukumu na akahudumia ujauzito ujauzito hadi mtoto alipozaliwa.

"Akaniambia na kuniuliza ikiwa niko tayari ama atoe. Kwa kuwa mimi ni Muislamu, kutoa mimba ni kushiriki  dhambi.  Sikuwa tayari kwa hayo. Niliamua ni njia ambayo mwenyezi Mungu aliamua kunipitisha. Kama mwanaume nilisimama kuhudumia kuhakikisha kwamba mimba inakuwa mpaka anazaliwa binti yangu mrembo, mpenzi wangu wa kwanza, Zuuh Konde. Jambo hilo lilimuumiza mtu ambaye nilikuwa naye kwa mahusiano, Sarah" Harmonize alisimulia.

Harmonize alisema alijaribu sana kuficha mtoto wake katika jitihada za kurejesha mahusiano mazuri na mke wake Sarah.

Mwanamuziki huyo alifichua utata mwingi ulizuka kuhusiana na uzazi wa malkia yule hadi akalazimika kufanya vipimo vya DNA baada ya kupata fununu kuwa huenda sio yeye baba mzazi.

"Tulipitia vitu vingi, DNA hivihivi kwa sababu kulikuwa na stori tofauti tofauti. Watu walikuwa wanaleta stori eti sijui mtoto si wangu. Lakini siku zote niliamini baba ni yule mtu ambaye amesimama na mtoto. Siri ya mtoto anayejua ni Mungu. Inawezekana ata mama ya mtoto asijue baba ni nani" Harmonize alisema.

Staa huyo wa Bongo alisema kuzaliwa kwa mtoto huyo kulisababisha mzozo mkubwa katika ndoa yake na Sarah  kwani walibishana kila siku kuhusu suala hilo. 

Hata hivyo ilifikia wakati akaweka mapenzi yake kwa bintiye kabla ya yale aliyokuwa nayo kwa mkewe  na hapo ndipo wakatengana.

"Iliishia kwa vita. Tulikuwa tunagombana kila siku. Tulikuwa tunagombana kila siku kuhusu mtoto. Ikafikia wakati nikamwambia nampenda mtoto wangu. Siwezi endelea kuficha mtoto wangu. Nitakuwa mzazi aina gani? Ulikuwa uamuzi wake ikabidi nimwambie  kama huo ndio mwisho wa mahusiano yetu ni sawa kwa sababu siwezi katupa damu yangu. Nilmwambia nataka kuwa baba mzuri. Ikafikia misuguano ya huku na kule mpaka mahusiano yetu ikaisha. Naamini Mungu alipanga tuwe pamoja kwa miaka minne. Zuuh ni mpenzi wangu wa kwanza. Ndio mtoto wangu wa pekee " Konde Boy alisema.

Harmonize amemuomba binti yake msamaha katika kibao chake cha kwanza kwenye albamu yake mpya.