"Alilia sana akiwa seli, OCS akamuonea huruma!" Ringtone adai alikuwa tayari kumlipia Eric Omondi dhamana ya Sh1.5M

Muhtasari

•Apoko alisema alikuwa ametoka kutoa pesa zile kwenye benki akikusudia kumlipia Omondi dhamana ila alipowasili katika kituo cha polisi akapata akiwa tayari ameachiliwa.

•Apoko alisema alikosa kuhudhuria maandamano yaliyokuwa yamepangwa na Omondi kwani yeye ni mwanamuziki wa nyimbo za injili na anapigana na mchekeshaji huyo kwa sababu anaendeleza uasherati.

Eric Omondi na Ringtone Apoko
Eric Omondi na Ringtone Apoko
Image: INSTAGRAM

Siku ya Jumanne habari kuhusu kukamatwa kwa mchekeshaji Eric Omondi alipokuwa anaongoza maandamano nje ya bunge la kitaifa ziligonga vichwa vya habari.

Msanii huyo asiyepungukiwa na drama alitiwa mbaroni asubuhi ya Jumanne alipokuwa ameongoza kikundi cha vijana kuandamana nje ya bunge la kitaifa wakidai marekebisho katika sekta ya muziki nchini.

Eric alikuwa ametoa wito kwa wasanii na waandishi wa habari washirikiane naye katika maandamano kuelekea bungeni kudai kuchezwa zaidi kwa sanaa ya Kenya na malipo bora kwa wasanii wakati wa tamasha.

Mchekeshaji huyo alipokamatwa alipelekwa katika kituo cha polisi cha Central ambako aliachiliwa baada ya kuzuiliwa kwa masaa machache.

Kikundi alichokuwa ameongoza kuandamana , na ambacho sanasana kilijumuisha vijana na wasanii chipukizi kililalamikia kukamatwa kwake na wakakita kambi nje ya kituo cha Central wakidai aachiliwe kwa haraka.

Baada ya Omondi kuachiliwa, mwanamuziki wa nyimbo za injili Ringtone Apoko alijitokeza akiwa amebeba bahasha iliyojaa mabunda ya noti za pesa ambazo alidai kuwa shilingi milioni moja unusu.

Alipokuwa anahutubia waandishi wa habari nje ya kituo cha polisi cha Central, Apoko alisema alikuwa ametoka kutoa pesa zile kwenye benki akikusudia kumlipia Omondi dhamana ila alipowasili katika kituo cha polisi akapata akiwa tayari ameachiliwa.

"Nimebeba milioni moja na nusu. Tulikuwa tunafikiri kwa makosa ambayo Eric Omondi amefanya ataachiliwa leo na dhamana ya nusu milioni kisha keshoye milioni. Yote nimebeba. Nimetumwa kama mwenye kiti nikuje nifanye hiyo kazi" Ringtone alisema.

Msanii huyo aliyezingirwa na utata mwingi kwenye taaluma yake ya muziki alisema Omondi aliachiliwa baada ya OCS kumwonea huruma kwani alilia sana alipokuwa korokoroni.

Ringtone alimshauri mchekeshaji huyo aache kupanga maandamano ya kupigania wanamuziki na badala yake aangazie wachekeshaji wenzake tu.

"Mambo  yote imefanyikia Eric Omondi nataka kukwambia tuko na wewe. Nilikuwa nimekuja kukulipia dhamana utoke lakini nimesikia kwamba ushaoka kwa sababu ulilia sana OCS akaona huruma. Umelia sana kwa cell wakaona hawataki  kushika mtoto. Wakati mwingine ukitaka kufanya maandamano ya maana ya kusaidia wasanii unawahusisha. Wewe ni mchekeshaji, ukitaka kufanya maandamano, fanya maandamano ya wachekeshaji" Alisema Apoko.

Apoko alisema alikosa kuhudhuria maandamano yaliyokuwa yamepangwa na Omondi kwani yeye ni mwanamuziki wa nyimbo za injili na anapigana na mchekeshaji huyo kwa sababu anaendeleza uasherati.