Harmonize afunguka kuhusu uhusiano wake na wapenzi wa zamani wa Diamond; Hamisa Mobetto, Zari na Tanasha

Muhtasari

•Harmonize amedai Diamond ndiye aliyepanga njama za kuharibu mahusiano yake na Sarah Michelloti pamoja na ya hivi karibuni na mwigizaji Fridah Kajala.

•Alifichua kwamba amewahi kukataa kupiga picha na Zari na vilevile akalenga kufanya kolabo na Hamissa Mobetto na Tanasha Donna ambao pia ni wanamuziki.

•Konde Boy alisema licha ya kuwa Zari, Hamisa na Tanasha ni mastaa na wana ufuasi mkubwa huwa anajitahidi sana kutojihusisha na jambo ambalo laweza kufanya ionekane kama kwamba anajaribu kumkomoa Diamond kwa yale alimfanyia.

Harmonize, Hamisa, Zari, Tanasha Donna
Harmonize, Hamisa, Zari, Tanasha Donna
Image: INSTAGRAM

Nyota wa muziki wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarufu kama Harmonize amefunguka kuhusu ugomvi wake na bosi wake wa zamani Diamond Platnumz.

Alipokuwa anahutubia waandishi wa habari punde baada ya kurejea Tanzania kutoka Marekani, Harmonize alimshtumu Diamond kwa kusababisha kuvunjika kwa mahusiano yake mawili ya hapo awali.

Harmonize alidai Diamond ndiye aliyepanga njama za kuharibu mahusiano yake na Sarah Michelloti pamoja na ya hivi karibuni na mwigizaji Fridah Kajala.

"Naamini asilimia mia, yeye amehusika kuvunja hayo mahusiano. Na hata suala la kuvunjisha video yangu ya uchi, alikuwa anataka kupiga ndege watatu kwa jiwe moja" Harmonize alisema.

Licha ya maovu yote ambayo alidai kutendewa na mmiliki wa Wasafi, Konde Boy amesema amekuwa akijizuia kabisa kulipiza kisasi.

Harmonize alisema hakuna uhasama wowote kati yake na wapenzi wa zamani wa Diamond, Hamisa Mobetto, Zari Hassan na Tanasha Donna huku akisema sababu za kutoonekana nao ni kwa sababu huwa anajiepusha kabisa na mambo ambayo yanaweza kufanya isemekane anamkomoa aliyekuwa mdosi wake.

Alifichua kwamba amewahi kukataa kupiga picha na Zari na vilevile akalenga kufanya kolabo na Hamissa Mobetto na Tanasha Donna ambao pia ni wanamuziki.

"Huwa najiepusha isije kusemekana  eti nimepiga picha nao kwa sababu nataka nimkomoe Diamond. Zari ni mtu mzuri, anaelewa sana. Wakati nilikuwa Afrika Kusini nikienda kurekodi video ya 'Bedroom'  nilienda kwa uwanja wa ndege kupanda KQ kugeuka nikamuona Zari. Aliniona wa kwanza akanisalimia alafu akatoa simu yake. Alipotoa simu nikamwambia nimeenda kufunga begi  alafu nikajificha nikaingia kwa ndege. Kumbe kwa bahati mbaya ama nzuri tulikuwa tunapanda ndege moja. Alikuja nikamwambia kwamba namheshimu na kupiga picha naye kungefurahisha mashabiki wake lakini singetaka ionekane vibaya. Nilimwambia sio eti mimi ni staa namvimbia nisipigwe picha naye (alianza kuwa staa kitambo hata kabla nijiunge na Wasafi) lakini singetaka apost picha yetu kwenye mitandao alafu isemekane eti nimepiga picha naye kwa sababu nina ugomvi na mzazi mwenzake.

Hamissa aliniomba tufanye wimbo nikamwambia nampenda sana na nasupport muziki wake lakini singeweza kufanya wimbo naye kwa sababu ingesemekana nafanya kwa ajili ya kumkomoa mzazi mwenzio. Vilevile Tanasha ashawahi kuniambia tufanye wimbo nikamwambia itafika muda lakini singeweza kwa wakati ule kwani ingeonekana nafanya kwa ajili ya kumkomoa mtu mwingine" Harmonize alisema.

Konde Boy alisema licha ya kuwa Zari, Hamisa na Tanasha ni mastaa na wana ufuasi mkubwa huwa anajitahidi sana kutojihusisha na jambo ambalo laweza kufanya ionekane kama kwamba anajaribu kumkomoa Diamond kwa yale alimfanyia.