"Mtoe muziki mzuri ambao naweza tumia nikitaka kufurahisha bibi" Babu Owino na Jaguar wahimiza wasanii wajitahidi zaidi

Muhtasari

•Babu amewahimiza wasanii wa Kenya kutoa muziki bora wenye uwezo wa kuyeyusha nyoyo za wasikilizaji huku akiapa kuendelea kuwaunga mkono.

•Jaguar kwa upande wake aliwahimiza wanamuziki kuangazia wasikilizaji wanaolenga kwenye nyimbo zao wakati wanapozitengeneza huku akiahidi kuwaunga mkono.

Babu Owino, Eric Omondi, Jaguar
Babu Owino, Eric Omondi, Jaguar
Image: INSTAGRAM// ERIC OMONDI

Siku ya Jumanne mchekeshaji Eric Omondi hatimaye aliweza kuwakabidhi wabunge  Babu Owino na Charles Njagua (Jaguar) muswada wake unaopendekeza vituo vya burudani viweze kucheza zaidi ya asilimia 75 ya muziki wa Kenya.

Omondi ambaye amekuwa akiangaziwa sana katika kipindi cha mwezi mmoja ambao umepita kufuatia drama nyingi zilizomzingira aliwasilisha muswada wake kwa wabunge hao wa muhula wa kwanza nje ya makao ya bunge la kitaifa huku akiwa ameandamana na kikundi cha wanahabari na wasanii chipukizi.

Mchekeshaji huyo aliwaomba Babu na Jaguar wahamasishe wabunge wenzao ili waweze kupitisha muswada huo ambao unalenga kuinua hadhi ya muziki wa Kenya.

Alipokuwa anakabidhiwa  muswada huo Babu Owino aliapa kuwasilisha muswada huo bungeni na kuhakikisha kuwa umeweza kupitishwa.

"Hatuwezi kubali kuangamiza sekta yetu ya muziki. Mimi kama mbunge kwa ushirikiano na mheshimiwa Jaguar na wabunge wengine vijana, na hata wazee kwa sababu huwa wanasikiliza muziki tungependa kuwashawishi wapitishe muswada huu ambao unapendeza vituo vya burudani  vicheze 75% ya muziki wa Kenya. Kwa kila klabu asilimia 75 ya muziki unafaa kuwa wa wasanii wa Kenya. Kila kituo cha redio, televisheni, mitandao ama hata machapisho ya gazeti ajenda kuu inafaa kuwa wanamuziki wa Kenya" Babu Owino alisema.

Mbunge huyo wa Embakasi Mashariki alipongeza juhudi za wanamuziki wa hapa nchini huku akidai kuwa yeye ni shabiki mkubwa wa nyimbo za Kenya.

Hata hivyo amewahimiza wasanii wa Kenya kutoa muziki bora wenye uwezo wa kuyeyusha nyoyo za wasikilizaji huku akiapa kuendelea kuwaunga mkono.

"Kufikia sasa tunaendelea vizuri. Tunawapongeza mnafanya kazi kubwa kama wasanii wa Kenya. Mimi hupenda muziki wa Kenya, uko sawa. Tutawaunga mkono. Kazi kwenu sasa, mhakikishe kuwa mmetoa  muziki mzuri ambao naweza cheza na kutumia nikitaka kufurahisha bibi" Babu alisema.

Jaguar kwa upande wake aliwahimiza wanamuziki kuangazia wasikilizaji wanaolenga kwenye nyimbo zao wakati wanapozitengeneza huku akiahidi kuwaunga mkono.

"Tutawaomba wabunge wote waunge mkono muswada ambao Babu atawasilisha bungeni. Baada ya kupititisha muswada, wasanii wasituangushe. Wahakikishe wametengeneza muziki ambao unaweza kushindana na wa Tanzania, Uganda na mataifa mengine" Alisema Jaguar.

Babu pia alisema ako tayari kuwa kwa video ya mwanamuziki yeyote wa Kenya kama 'vixen' kama alivyokuwepo kwenye video ya wimbo 'Adhiambo' wa Bahati na Prince Indah.