Kabi Wajesus ataja sababu za kumtambulisha binti yake, Abby mitandaoni

Muhtasari

•Kabi amesema alipiga hatua hiyo kudhihirisha wazi kuwa anajivunia binti yake na anampenda sana licha ya utata uliozingira kuzaliwa kwake.

•Alisema  licha ya kuwa anafaa kuona binti yake kila baada ya wiki mbili, hilo halijawezekana sana kwa kuwa kumekuwa na vuta nikuvute kati yake na mama Abby.

Image: INSTAGRAM// MILLY WA JESUS

Takriban siku mbili zilizopita Kabi Wajesus alimtambulisha binti yake wa miaka saba  Abby  mitandaoni kwa mara ya kwanza.

Kabi amesema alipiga hatua hiyo kudhihirisha wazi kuwa anajivunia binti yake na anampenda sana licha ya utata uliozingira kuzaliwa kwake.

Alipokuwa kwenye mahojiano na Mungai Eve, Kabi alisema hangependa binti yake akue akijiona kama kwamba yeye ni siri kwake ama kwa jamii.

"Ningependa binti yangu ajue kuwa yeye sio siri kwangu,kwa jamii  na yeye sio kitu kibaya. Nampenda na nimemkubali. Ningependa awe sehemu ya maisha yangu kama  watoto wengine ambao watakuja baada yake. Sitaki akue ashangae mbona Taji huwa pale na mimi sijawahi kuwa. Nataka  ajue nampenda licha ya mazingira ya kuzaliwa kwake" Kabi alisema.

Kabi aweka wazi amekuwa akiwajibikia binti yake tangu wakati vipimo vya DNA vilibaini kuwa ndiye baba mzazi.

Alipuuzilia mbali madai ya mama Abby kuwa alikosa kulipa karo ya shule  ya binti yao huku akidai alilazimika kumbadilisha shule kwa kuwa mama yake alishindwa kugharamia karo nusu aliyotengewa.

"Nimelipa karo ya Abby kutoka mwezi Mei baada ya matokeo ya DNA kutoka. Nililipa muhula wa mwisho wa gredi ya kwanza zilikuwa takriban 58, 000. Mara ya pili korti iliamuru tulipe nusu nusu, nililipa 30,000 yangu sijui kama yeye alilipa. Katika muhula wa tatu mimi ndiye nagharamia karo ya shule ya binti yangu kikamilifu" Alisema Kabi.

Alisema  licha ya kuwa anafaa kuona binti yake kila baada ya wiki mbili, hilo halijawezekana sana kwa kuwa kumekuwa na vuta nikuvute kati yake na mama Abby.

"Nitaendelea kukazania hilo. Najua sio rahisi kwa hivyo sitarajii ukamilifu. Sitaraji kumuona kila wakati. Saa hii ni ngumu  kumuona lakini nikipata nafasi nitahakikisha tumekuwa na wakati mzuri pamoja"  Kabi alisema.

Kabi alikiri kuwa ni kweli mama ya Abby anayefahamika kama Shiko ni binamu yake huku akieleza kuwa babu zao ni ndugu.

Alisema kwa sasa mzazi huyo tayari ameolewa kwingine na wamebarikiwa na watoto wengine wawili. Alieleza walielewana na wanandoa hao kuhusu jinsi wangeshirikiana katika malezi.