"Hana taste bado, mimi ndio huonja chakula chake!" Nana Owiti azungumza kuhusu afya ya mumewe, King Kaka

Muhtasari

•Alisema hali hiyo inamlazimu aonje chakula chake kabla ya kumkabidhi kwa sababu kuna baadhi ya viungo vya chakula ambavyo hafai kuwa anakula kwani mfumo wake wa utumbo ulikuwa umeathirika .

•Bi Owiti aliweka wazi kwamba mumewe aliathiriwa na dawa ambazo alipatiwa baada ya kupimwa vibaya.

Image: INSTAGRAM// KING KAKA

Mtangazaji Nana Owiti ambaye ni mke wa rapa Kennedy Ombima almaarufu kama King Kaka amefahamisha mashabiki kuhusu afya ya mumewe kwa sasa.

Akiwa kwenye mahojiano na Mungai Eve wakati wa hafla ya kuzindua EP ya King Kaka, Bi. Owiti alifichua kwamba afya ya mwanamuziki huyo imeimarikwa kwa sasa.

Owiti hata hivyo alisema hisia ya ladha ya mumewe bado haijarejea tangu alipoipoteza takriban miezi sita iliyopita wakati alianza kuugua.

Alisema hali hiyo inamlazimu aonje chakula chake kabla ya kumkabidhi kwa sababu kuna baadhi ya viungo vya chakula ambavyo hafai kuwa anakula kwani mfumo wake wa utumbo ulikuwa umeathirika .

"Ako sawa. Kilichobaki ni kwamba bado hana hisia ya ladha. Mimi ndio huwa naonja chakula chake tangu alipoanza kuugua, imekuwa miezi. Lazima nionje chakula chake ndio kisiwe na viungo vingi kwa sababu bado ako katika safari ya kupona. Mfumo wake wa utumbo kutoka kwa koo ulikuwa umeathirika kwa hivyo lazima tuchukue tahadhari.  Hawezi kula pilipili, hawezi kula viungo,kuna vitu vingi ambavyo hafai kuwa anakula" Owiti alisema.

Mama huyo wa watoto wawili aliweka wazi kwamba mumewe aliathiriwa na dawa ambazo alipatiwa baada ya kupimwa vibaya.

Alisema King Kaka bado alikuwa anaendelea kutunga na kutengeneza nyimbo hata alipokuwa anaugua kwa zaidi ya miezi mitatu.

"Yeye si mtu ambaye hukaa tu. Alikuwa mgonjwa kabisa na angeniambia hajiskii akiwa na nguvu. Nilikuwa namwambia ni kawaida kuishiwa na nguvu mtu akiwa mgonjwa" Alisema.

Mwanamuziki huyo ameendelea kupata afueni na tayari amerejesha uzito mwingi wa mwili ambao alikuwa amepoteza.