Itagharimu Sh850,000 kwa rapa Diana B kutumbuiza katika hafla moja: - Bahati adai

Muhtasari

• Bahati alimtaja mkewe kama rapa bora zaidi huku akisema ada yake kutumbuiza katika hafla yoyote itakuwa shilingi 850,000.

•Alifichua kuwa mkewe tayari ametengeneza nyimbo nne na hata kurekodi video ambazo zitakuwa zinatolewa hivi karibuni.

•Diana alithibitisha kuwa aliandika wimbo 'Hatutaachana' mwenyewe wala si kuandikiwa huku akiahidi kuachilia vibap vingine hivi karibuni.

Image: INSTAGRAM// DIANA MARUA

Gumzo ambayo imekuwa ikienea sana mitandaoni katika kipindi cha siku chache zilizopita ni kuhusu hatua ya mke wa Bahati, Diana Marua kujitosa kwenye sekta ya muziki.

Diana Marua alizinduliwa kama mwanamuziki wa nyimbo za kufoka siku ya Jumapili katika hafla iliyohudhuriwa na wasanii na watu mashuhuri akijitambulishwa kwa jina la jukwaani kama Diana B.

Malkia huyo mwenye umri wa miaka 32 alitoa kibao chake cha kwanza 'Hatutaachana' siku ya Jumatatu na kiliweza kupokea watazamaji wengi kweli masaa punde baada ya kuachiliwa.

Akiwa kwenye mahojiano na Mpasho, Bahati alimtaja mkewe kama rapa bora zaidi huku akisema ada yake kutumbuiza katika hafla yoyote itakuwa shilingi 850,000.

"Yeye ni rapa. Ada yake kujitokeza kwa hafla akiwa mwanavlogu tu ni shilingi laki tano. Usimamizi ulikuwa unapendekeza shilingi 850, 000 kila anapotumbuiza kwa sasa. Lazima apate pesa alipe KRA.. Yeye ndiye bora zaidi, yeye ni wa kipekee . Kwa sasa yeye ndiye rapa bora zaidi wa kike nchini, niamini" Bahati alisema.

Mwanamuziki huyo ambaye amekuwa akivuma kwa zaidi ya miaka saba pia alifichua kuwa mkewe tayari ametengeneza nyimbo nne na hata kurekodi video ambazo zitakuwa zinatolewa hivi karibuni.

Aliweka wazi kuwa Diana B atakuwa na usimamizi wake binafsi kimuziki kando na ule wake huku akisema  hata lebo ya Diamond Platnumz, Wasafi iko huru kumsajili.

"Yeye ni mwanamuziki huru. Anaweza enda kokote. Hata anaweza sajiliwa na Wasafi. Mimi sifanyi lebo, nitamuunga mkono tu na nihakikishe ameshaurika vizuri. Ako na usimamizi wake binafsi lakini kwa sasa meneja wangu anamsimamia upande wa muziki.. Ako na nyimbo nne ambazo ziko na video tayari, tulitaka kuzindua mbili lakini tukaona tuache tu. Alianza na tutaacha" Bahati alisema.

Diana alithibitisha kuwa aliandika wimbo 'Hatutaachana' mwenyewe wala si kuandikiwa huku akiahidi kuachilia vibap vingine hivi karibuni.