"Kuna raha kubwa katika uzazi" Vera Sidika akiri anajivunia hatua ya kuwa mama

Muhtasari

•Malkia huyo mwenye umri wa miaka 31 amedai kupata mtoto kwake ndio uamuzi bora amewahi kufanya maishani.

Image: INSTAGRAM// VERA SIDIKA

Mwanasoshalaiti mashuhuri Vera Sidika amekiri kufurahishwa sana na hali yake mpya ya kuwa mzazi.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, malkia huyo mwenye umri wa miaka 31 amedai kupata mtoto kwake ndio uamuzi bora amewahi kufanya maishani.

Vera amesema ujio wa bintiye, Asia Brown takriban mwezi mmoja unusu uliopita ulikuwa baraka kubwa kwake huku akisisitiza anapendezwa sana na kifungua mimba huyo wake.

“Kupata mtoto ndio uamuzi bora nimewahi kufanya maishani!!! Waah, hamkuniambia kuna raha kubwa katika uzazi. Napendezwa sana na Asia” Vera amesema.

Vera alimkaribisha mtoto wake wa kwanza na mpenziwe Brown Mauzo mnamo Oktoba 20, 2021 wakati taifa lote lilikuwa linaadhimisha siku ya Mashujaa Day.

Mwanasoshalaiti huyo alijifungua mtoto wa kike kwa njia ya upasuaji almarufu kama CS kama  ilivyokuwa mapenzi yake.

Hivi majuzi Vera alifichua hakuhisi uchungu wowote alipokuwa anafanyiwa upasuaji na hata baada ya kujifungua.

Vera alisema upasuaji ambao alifanyiwa haukumwathiri kwa namna yoyote huku akiweka wazi hakuna yeyote aliyemchukulia kama mgonjwa kwa kuwa hakuwa na maumivu yoyote.

"Hakuna aliyenichukulia kama mgonjwa baada ya CS kwa kuwa nilikuwa tu kama kawaida yangu. Kwa wakati mwingine huwa natamani ningefanya kuwa mgonjwa ama nahisi uchungu ili nipewe huduma zaidi kama mtu mgonjwa na nihurumiwe... Nikiwa hospitalini nilikuwa napewa dawa za kutuliza uchungu  zenye nguvu kila wakati kwa hivyo sikuhisi uchungu wowote. Hata niliweza kukaa chini kwa kitanda cha hospitali masaa machache baada ya upasuaji. Sikula chochote baada ya masaa 6-7. Nilichohisi ni kiu na walipunguza kiasi cha maji ambacho nilifaa kunywa" Alisema Vera.

Vera alisema ako tayari kubeba ujauzito mwingine huku akidai mpenzi wake amekuwa akimshinikiza wapate mtoto wa pili hivi karibuni.