“Niko tayari kukuchukua, kukupenda pamoja na bintiyo!” B Classic atamani kujaza pengo lililoachwa na Mulamwah

Muhtasari

•Mwanamuziki huyo mzaliwa wa kaunti ya Taita Taveta  alisema ako tayari kumchukua mama Keilah, kumpenda na kumthamini pamoja na bintiye wa miezi miwili.

Mulamwah, Carrol Sonnie na B Classic
Mulamwah, Carrol Sonnie na B Classic
Image: INSTAGRAM

Siku ya Jumatatu Bi. Caroline Muthoni alijitosa mitandaoni kutangaza kutengana kwake na mchekeshaji David Oyando almaarufu kama Mulamwah.

Bi Muthoni ambaye anafahamika zaidi kama Carol Sonnie alitangaza walifanya makubaliano ya pamoja kutengana huku akimshukuru baba ya binti wake kwa kipindi cha miaka minne ambacho wamekuwa pamoja.

"Hii ni kuweka wazi kuwa mimi na Mulamwah hatuko pamoja tena. Sote tumekubaliana na kuamua kuachana kwa sababu zinazojulikana kwetu. Asante sana kwa upendo na usaidizi mliotupa kwa miaka hiyo 4, mimi binafsi sichukulii kawaida.

Kwa mulamwah, Asante sana kwa kuniruhusu kuwa sehemu ya maisha yako kwa miaka hiyo.  Nashukuru sana na nitahifadhi kumbukumbu milele. Katika hatua yako inayofuata maishani, sikutakii kingine ila bora.Endelea kushinda na Mungu akubarikikatika  kila hatua ya maisha yako" Muthoni aliandika.

Tangazo hilo lilipokelewa kwa hisia tofauti baadhi ya wanamitandao wakilitilia shaka na kudai ni kiki huku wengine wakiamini kufuatia matendo yao ya hivi majuzi mitandaoni.

Mwanamuziki Dennis Manja almaarufu kama B Classic kwa upande wake alitumia fursa ile kujipendekeza na kujitetea kwa Muthoni.

B Classic alikosoa Mulamwah kufuatia utengano huo huku akijitolea kujaza nafasi iliyoachwa wazi na mchekeshaji huyo.

Mwanamuziki huyo mzaliwa wa kaunti ya Taita Taveta  alisema ako tayari kumchukua mama Keilah, kumpenda na kumthamini pamoja na bintiye wa miezi miwili.

"Carol SONNIE kuanzia hatua hii mbele, upendo unaohisi hautaamuliwa na hali yako. Imeniumiza sana kusema kweli jinsi Mulamwah ameshughulikia haya yote, Ila nakuhakikishia niko tayari kukuchukua, kukupenda na kukuthamini kwa moyo wangu wote pamoja na binti yako❤️❤️❤️.Ntakupenda Na Moyo Wangu Wote ❤️💞🌹❣️" Alisema B Classic kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Haya yanajiri miezi miwili tu baada ya Mulamwah na Muthoni kukaribisha mtoto wao wa kwanza Keilah Oyando.

Mwaka uliopita walikuwa wametengana tena kwa kipindi kisha wakarudiana ila hawakufichua kilichokuwa kimewatengisha