"Karibu nyumbani, nimekumiss kinyama!" Nyota Ndogo atembelewa na mumewe mzungu kwa mara nyingine

Muhtasari

•Mwanamuziki huyo kutoka Pwani  alimlaki raia huyo wa Udenmarki katika uwanja wa ndege wa JKIA siku ya Jumanne huku akikiri alivyokuwa amempeza kishenzi.

• Mdenmarki huyo alikuwa ametembea tena nchini mwishoni mwa mwezi Septemba na kukaa siku kadhaa kabla ya kurudi Ulaya.

Image: INSTAGRAM// NYOTA NDOGO

Mwanamuziki Mwanaisha Abdalla almaarufu kama Nyota Ndogo ni mwenye bashasha  tele  huku akimkaribisha mumewe Henning Nielsen  nchini  kwa  mara nyingine mwaka huu.

Nyota Ndogo alijitosa kwenye mtandao wa Instagram  asubuhi ya Jumatano kutangaza kuhusu kuwasili kwa mumewe na kuthibitisha kwa picha kadhaa maridadi alizopakia ambazo walipigwa pamoja.

Mwanamuziki huyo kutoka Pwani  alimlaki raia huyo wa Udenmarki katika uwanja wa ndege wa JKIA siku ya Jumanne huku akikiri jinsi alivyokuwa amempeza kishenzi.

"Mapenzi ni kitu kizuri sana. Bwana akitokea  umependa, mpe 100%. Karibu nyumbani mume wangu, nimekumiss kinyama" Nyota aliandika chini ya picha zake na mumewe alizopakia.

Hii ni mara ya pili kwa bwana Nielsen kumtembelea mke wake mwaka huu. Mdenmarki huyo alikuwa ametembea tena nchini mwishoni mwa mwezi Septemba na kukaa siku kadhaa kabla ya kurudi Ulaya.

Wiki chache zilizopita, msanii huyo alizama mtandaoni kumsihi mumewe arudi huku akimweleza jinsi alivyokuwa anampeza kupindukia.

"Nimemiss jasho lako hebu njoo" Nyota Ndogo alimwandikia mumewe kupitia ukurasa wa Instagram.

Ama kweli Mola kamtunuku mama huyo wa watoto wawili na mume anayemsikiza kwani hata mwezi haujauisha kabla ajibu ombi lake.