Rue Baby aahirisha hafla ya kusherehekea kuhitimu kwake kufuatia ugonjwa wa mama yake Akothee

Muhtasari

•Rue Baby ambaye alihitimu kutoka chuo kikuu cha Strathmore wiki iliyopita amesema hatua ya kuahirisha sherehe zake imeafikiwa ili kupatia mamake muda wa kupata afueni huku akiomba kusaidiwa kumshawishi mwanamuziki huyo atulie kwanza.

•Akothee ameweka wazi kwamba bintiye alifanya maamuzi ya kuahirisha hafla hiyo pekee yake bila kumuomba ushauri. 

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Binti mzaliwa wa pili wa mwanamuziki na mfanyibiashara maarufu Esther Akoth (Akothee) , Rue Baby ameahirisha hafla ya kusherehekea kuhitimu kwake kutoka chuo kikuu ambayo ilikuwa imepangwa kufanyika siku ya Jumamosi. 

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, kipusa huyo mwenye umri wa miaka 23 ametangaza kwamba mama yake anaugua.

Rue Baby ambaye alihitimu kutoka chuo kikuu cha Strathmore wiki iliyopita amesema hatua ya kuahirisha sherehe zake imeafikiwa ili kupatia mamake muda wa kupata afueni huku akiomba kusaidiwa kumshawishi mwanamuziki huyo atulie kwanza.

"@akotheekenya hii inaelekezwa kwako. Najua itakushangaza lakini hauko sawa yawa mama. Kuna mtu anaweza kunisaidia kumfunga ili awe sawa kwanza .. tunaweza kufanya sherehe baadaye. @drofweneke naomba usaidizi tafadhali. Hadi taarifa zaidi kutolewa" Rue Baby aliandika.

Akothee ameweka wazi kwamba bintiye alifanya maamuzi ya kuahirisha hafla hiyo pekee yake bila kumuomba ushauri. 

Msanii huyo amefichua ni ngumu kuamuru binti yake kufanya jambo lolote huku akidai kuwa ata amekataa kuchukua simu zake baada ya kupiga hatua ile.

"Mmoja wa watoto wangu mgumu zaidi! Huwezi kumuamuru, anafanya mambo yake kwa njia zake, na lazima ifanywe kwa atakavyo! Vivyo hivyo kipusa huyu aliahirisha sherehe yake ya kuhitimu bila kuniambia! hapokei simu zangu. Ni kutuma tu meseji ati nipone kwanza 🤔🤔 Vile vile mtu anaweza kumwambia @rue.baby atupe tarehe nyingine ya upendeleo wake basi 🤷🙏 Nataka kumsherehekea kwa kiasi kikubwa ,@rue.baby asayi nyakwar ma , hizi ni sherehe za pekee kwangu 🙏" Akothee amesema

Kwa muda sasa hali ya afya ya Akothee haijakuwa imara kabisa.

Mwezi jana mama huyo wa watoto watano alikuwa amelazwa hospitalini ambako alihudumiwa kwa siku kadhaa kabla ya kuruhusiwa kuenda nyumbani.

Wiki iliyopita mwanamuziki huyo alieleza kwamba ugonjwa ambao umemwathiri kwa muda umemsababishia uvimbe ambao unafanya aonekane mnene zaidi. Alisema maumivu ambayo amekuwa akipata mwilini yamemfanya kukosa usingizi kiasi cha kwamba amekuwa akihofia kuingia kitandani.

'Usikutane na kuanza kuniambia jinsi nilivyo mnene, nina hali ya kiafya, nimevimba kutokana na kuhangaika na maumivu ya kukosa usingizi, naogopa kwenda kulala maana ninaamka na ganzi kwenye vidole vyangu, hali hii inanitisha. Namuonea huruma jamaa yangu mmoja wa karibu aliyesema najifanya  bado sijui nimwambie nini " Akothee amesema.

Akothee aliwasuta vikali wanaomtakia maovu na kuongea mabaya kuhusu hali yake huku  akidai sanasana watu wenye tabia ile huwa wale wa karibu.