(+Video) Guardian Angel na mpenziwe Esther Musila wajenga nyumba ya familia

Mradi huo umefikia hatua ya ujenzi wa kuta.

Muhtasari

•Guardian Angel alithibitisha hatua hiyo  kupitia ukurasa wake wa Instagram ambapo alipakia video inayoonyesha akikagua mradi wa ujenzi unaoendelea.

•Mwanamuziki huyo alipuuzilia mbali madai kuwa alijitosa kwenye mahusiano na Bi Musila kwa sababu za kifedha.

Image: INSTAGRAM// GUARDIAN ANGEL

Kila uchao mwanamuziki mashuhuri wa nyimbo za injili Guardian Angel na mke wake Esther Musila wameendelea kuwathibitisha wanaotilia penzi lao shaka kuwa wamekosea na kuonyesha uzito wa mahusiano yao huku  sasa wakionekana kupiga hatua ya kujenga makao ya kuishi pamoja na kusherehekea ndoa yao.

Guardian Angel alithibitisha hatua hiyo  kupitia ukurasa wake wa Instagram ambapo alipakia video inayoonyesha akikagua mradi wa ujenzi unaoendelea.

Katika video hiyo, mradi huo mkubwa ulionekana kuendelea vizuri huku ukiwa umefikia hatua ya ujenzi wa kuta.

"Mungu mwaminifu. Mungu si binadamu!" Guardian Angel aliandika chini ya video aliyopakia.

Mashabiki wake walifurika chini ya chapisho lake na jumbe kochokocho za pongezi kufuatia hatua kubwa aliyopiga.

@dkkwenyebeat Yeye ni mwaminifu

@wanderi75 Nitakupigia makofi hadi itakapofika wakati wangu

@chep_mariana Mungu mwaminifu kweli

@kevochimusiqofficial utukufu kwa Mungu

Mwezi uliopita Guardian Angel alipokuwa anazindua albamu yake alijipiga kifua kwamba fedha ambazo ameweza kukusanya mpaka sasa zinaweza kumudumisha pamoja na mkewe maisha yao yote hata akiamua kuacha muziki.

Mwanamuziki huyo alipuuzilia mbali madai kuwa alijitosa kwenye mahusiano na Bi Musila kwa sababu za kifedha.

Wawili hao wamekuwa wakikosolewa sana mitandaoni kufuatia pengo kubwa katika umri wao. Guardian Angel ana umri wa miaka 31 ilhali mkewe ana umri wa miaka 51.