"Huwa tunapigana" Kabi na Milly Wajesus wafunguka kuhusu ndoa yao ya miaka minne

Muhtasari

•Wawili hao walisema ndoa yao haijakuwa paradiso kila wakati na kukiri kwamba huwa wanatofautiana mara kwa mara.

•Milly alisema safari yao ya ndoa imekuwa nzuri huku akiweka wazi kuwa mumewe amekuwa mwaminifu sana kwake tangu walipofunga ndoa.

•Kabi alisema anamwamini sana mke wake na kudai kwamba hawezi kupatwa na wasiwasi wowote kumhusu hata akimuacha miongoni mwa wanaume wengine.

Kabi Wajesus na Milly Wajesus
Kabi Wajesus na Milly Wajesus
Image: INSTAGRMA// KABI WAJESUS

Mnamo siku ya Alhamisi wanandoa mashuhuri Peter Kabi na Millicent Wambui walifunguka kuhusu mambo mbalimbali kuhusiana na ndoa yao.

Wazazi hao wa mtoto mmoja walitumia mtandao wa YouTube kujibu maswali ya mashabiki wao  kuhusu ndoa yao ya miaka minne.

Wawili hao walisema ndoa yao haijakuwa paradiso kila wakati na kukiri kwamba huwa wanatofautiana mara kwa mara. Hata hivyo waliweka wazi kwamba huwa hawapigani vita vya kimwili.

"Katika mwaka wa kwanza wa ndoa ungetuuliza  kama huwa tunapigana tungesema la, mwaka wa pili pia tungesema hapana, mwaka wa tatu tungesema ni kama huwa  tunapigana kidogo, mwaka wa nne  mngeuliza ni nani mpiganaji bora zaidi ama nani hushinda tunapopigana. Kwa kweli huwa  tunapigana, sio vita vya kimwili lakini huwa tunakosa kukubaliana kwa mambo fulani" Milly alisema.

Alisema sasa hivi wanakosa kukubaliana katika masuala mengi kwa kuwa kuna mambo mengi yanaendelea ikiwemo biashara ya na  ujenzi wa nyumba. Alisema huwa hawaruhusu kutofautiana kwao kuwatenganishe.

Milly alisema safari yao ya ndoa imekuwa nzuri huku akiweka wazi kuwa mumewe amekuwa mwaminifu sana kwake tangu walipofunga ndoa.

"Nimeget over wapenzi wa zamani. Ukipata kitu kizuri lazima usahau yale mabaya... Acha niseme kufikia sasa Kabi amekuwa mume mwaminifu sana. Siwezi kuzungumza kuhusu suala la udanganyifu kutokana na kupitia. Najua  watu walio kwa ndoa na watu ambao walicheza karata nje ya ndoa hapo awali" Alisema.

Kabi alisema anamwamini sana mke wake na kudai kwamba hawezi kupatwa na wasiwasi wowote kumhusu hata akimuacha miongoni mwa wanaume wengine.

"Mimi hujiamini. Mimi  siwezi kuwa na wasiwasi. Najua msichana huyu ananipenda, anajua nampenda. Mimi ni mwaminifu kwake, namwamini. Siwezi ogopa kitu chochote, ata nikimuacha na mwanaume kwa nyumba siwezi ogopa" Alisema.

Wawili hao wamekuwa katika ndoa kwa kipindi cha minne na wamebarikiwa na mtoto mmoja tayari.