"Washerati ndio wako na homa!" Ringtone Apoko atoa hisia zake kuhusu homa iliyoshambulia Wakenya

Muhtasari

•Kulingana na Apoko, wote ambao wameshambuliwa na homa hiyo ya ajabu ni wenye dhambi ilhali walio watakatifu wanaendelea kufurahia afya njema

•Katika kipindi cha takriban wiki moja ambacho kimepita maelfu ya Wakenya wamekuwa wakilalamika kuhusu homa kali ambayo imewakosesha amani usiku na mchana.

Image: INSTAGRAM// RINGTONE APOKO

Mwenyekiti wa muungano wa wanamuziki wa Injili wa kujibandika Ringtone Apoko amejitokeza kutoa hisia zake kuhusiana na homa ambayo imekuwa ikihangaisha kikundi kikubwa cha Wakenya katika siku za hivi majuzi.

Katika kipindi cha takriban wiki moja ambacho kimepita maelfu ya Wakenya wamekuwa wakilalamika kuhusu homa kali ambayo imewakosesha amani usiku na mchana.

Kulingana na Apoko, wote ambao wameshambuliwa na homa hiyo ya ajabu ni wenye dhambi ilhali walio watakatifu wanaendelea kufurahia afya njema.

"Nataka niwaambie saa hii wale watu wote wako na homa hii Nairobi ni wenye dhambi. Washerati ndio wako na homa juu ya kubusu ovyoovyo. Mbona sisi watu wazuri, watu wa Mungu, Watoto wasafi,watoto hatuna maneno tunaheshimu sheria za Mungu hatuna homa?!" Apoko alisema kwenye video ambayo alipakia Instagram.

Wakenya wameendelea kushangazwa na homa ambayo imelipuka kwa kiwango kikubwa katika kipindi cha wiki moja ambacho kimepita. 

Wakenya wengi wamekuwa wakilalamikia dalili za mafua ikiwa ni pamoja na kutokwa na kamasi, homa, kupiga chafya na kuumwa na kichwa.

Siku ya Alhamisi, KEMRI ilithibitisha mlipuko wa homa ya virusi vya mafua aina ya Influenza hapa nchini. 

Kemri ilisema kuwa sampuli kati ya 36 zilizopimwa, nne zilipatikana na homa ya influenza A.