"Willy Paul amesimama kwa sababu ya Bahati, Hana pesa za kampeni!" Ringtone Apoko adai

Muhtasari

•Kulingana na Apoko, Bahati ndiye alitangulia kutangaza azma ya kuwania kiti cha ubunge cha Mathare na Willy Paul alipiga hatua ile kwa sababu ya ugomvi wao.

•Msanii huyo wa nyimbo za injili anayefahamika kwa kujipiga kifua kuhusu utajiri wake mkubwa alidai Willy Paul hana fedha za kufanya kampeni huku akimshauri aangazie muziki aachane na siasa.

Image: INSTAGRAM// RINGTONE APOKO, WILLY PAUL

Hivi majuzi mwanamuziki Wilson Radido almaarufu kama Willy Paul ametangaza azma yake ya kuwania kiti cha ubunge cha Mathare.

Mwanamuziki huyo asiyepungukiwa na drama katika taaluma yake ya usanii alitangaza azma yake kupitia ukurasa wake wa Instagram.

"Je, mko tayari Mathare? Tulete mabadiliko hayo," Willy Paul aliandika na kuambatanisha ujumbe wake na picha ya bango lenye sura yake na maandishi "Willy Paul, Mathare MP 2022."

Wakenya wameendelea kutoa hisia tofauti kuhusiana na hatua hiyo ya Willy Paul ambayo imejiri wiki chache tu baada ya madai kuwa alijaribu kumbaka mke wa Bahati, Diana Marua kuvuma mitandaoni.

Mwenyekiti wa baraza la wanamuziki wa injili wa kujibandika Ringtone Apoko hajachelewa kutoa kauli yake kuhusiana na hatua ya Willy Paul.

Akizungumza na Mungai Eve, Apoko alisema Willy Paul hana mpango wa kuwania kiti hicho na alitoa tangazo ili kumchanganya akili Bahati.

Kulingana na Apoko, Bahati ndiye alitangulia kutangaza azma ya kuwania kiti cha ubunge cha Mathare na hatua  ya Willy Paul alichangiwa na ugomvi wao.

"Willy Paul amesimama kwa sababu ya Bahati. Yeye ndiye alikuwa ashatangaza anasimama Mathare kwa hivyo Willy Paul anampiga tu Bahati. Bahati alikuwa ametuambia anasimama Mathare, ukiona Willy Paul akitangaza ni hizo beef zao tu. Willy Paul hatasimama, anataka tu kuchanganya Bahati. Anataka tu kumharibia" Ringtone alisema.

Msanii huyo wa nyimbo za injili anayefahamika kwa kujipiga kifua kuhusu utajiri wake mkubwa alidai Willy Paul hana fedha za kufanya kampeni huku akimshauri aangazie muziki aachane na siasa.

Ringtone alisema licha ya kuwa yeye ni tajiri mkubwa na Willy Paul ni rafiki yake hawezi kufadhili kampeni zake kwa kuwa anafahamu anafanya mzaha tu.

"Willy Paul akuwe tu serious na muziki, aachane na mambo ya siasa. Hana pesa za kampeni, hatuwezi mfadhili kwa sababu hayuko serious. Willy Paul ana talanta kubwa, aimbe tu" Alisema.

Apoko hata hivyo alisifia sana talanta ya Willy Paul katika muziki huku akidai hakuna msanii yeyote wa nyimbo za kidunia anayeweza kumshinda iwapo atamakinika zaidi. Alisema hata  staa wa Bongo Diamond Platnumz ni kivuli kwa Paul.