Karen Nyamu azungumzia kufanya kampeni akiwa mjamzito na Samidoh kutotumbuiza katika kampeni zake

Muhtasari

• Nyamu alisisitiza kuwa hali yake ya ujauzito haitapunguza kasi ya kampeni zake.

•Alieleza kuwa Samidoh sio mfuasi wa chama cha UDA ambacho anatazamia kutumia kuwania kiti cha useneta, jambo ambalo huenda likamzuia nyota huyo wa Mugithi kujihusisha katika kampeni zake.

Karen Nyamu akihutubia wafanyibiashara wadogo kutoka kaunti ya Nairobi katika makao ya naibu rais William Ruto mapema mwezi Desemba.
Karen Nyamu akihutubia wafanyibiashara wadogo kutoka kaunti ya Nairobi katika makao ya naibu rais William Ruto mapema mwezi Desemba.
Image: INSTAGRAM// KAREN NYAMU

Wakili na mwanasiasa mashuhuri Karen Nyamu amethibitisha atakuwa kwenye kinyang'anyiro cha kiti cha useneta  cha Nairobi.

Akiwa kwenye mahojiano na Mpasho, Nyamu alisisitiza kuwa hali yake ya ujauzito haitapunguza kasi ya kampeni zake.

Mgombeaji huyo wa kiti cha mwakilishi wa wanawake wa kaunti ya Nairobi katika chaguzi za 2017 alisema hali ya ujauzito sio geni kwake huku akidai kuwa hapo awali alipokuwa katika hali ile alifanya kazi zake kama kawaida bila tatizo lolote hadi siku ya kujifungua.

"Nimekuwa mjamzito hapo awali na sikuacha kufanya kazi hadi dakika ya mwisho kabisa kabla nijifungue mtoto. Sioni utofauti wowote. Kampeni ni kazi tu. Nimekuwa nikifanya kazi nikiwa mjamzito hadi siku ya mwisho kabla nipate mtoto" Nyamu alisema.

Wakili huyo alipoulizwa iwapo baba wa mtoto wake wa pili na ambaye wanatarajia mtoto mwingine naye, Samidoh, atatumbuiza katika kampeni zake alidai kuwa hatahitaji wasanii wa  kutumbuiza atakapokuwa anajipigia debe.

Nyamu hata hivyo alifichua huwa anaomba nyota huyo wa Mugithi ushauri mara kwa mara kwani  kwani yeye ni baba wa watoto wake, rafiki wake wa karibu, ni mwenye maarifa na anaelewa watu sana.

"Sihitaji wasanii kutumbuiza katika kampeni zangu. Yeye ni baba wa watoto wangu, yeye ni rafiki wangu mzuri. Huwa namuomba ushauri, ana maarifa mengi, anaelewa watu kwa sababu huwa anashughulika na umma sana. Huwa namuomba ushauri sana na yeye husaidia sana. Kwa kutumbuiza, sidhani kuna wakati nitahitaji wasanii kutumbuiza katika kampeni zangu" Alisema.

Hali kadhalika Nyamu alieleza kuwa Samidoh sio mfuasi wa chama cha UDA ambacho anatazamia kutumia kuwania kiti cha useneta, jambo ambalo huenda likamzuia nyota huyo wa Mugithi kujihusisha katika kampeni zake.