"Nitafanya kila kitu kumlinda binti yangu!" Willy Paul ajivunia bintiye na Baby Mama wake Mrusi

Muhtasari

•Willy Paul alitangaza kuzaliwa kwa binti yake, Sonya na mwanamitindo huyo wa Kirusi mwishoni mwa mwaka jana.

Image: INSTAGRAM// WILLY PAUL

Siku ya Alhamisi mwanamuziki Wilson Radido almaarufu kama Willy Paul alipakia video ya Baby Mama wake mzungu na bintiye kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Willy Paul ambaye amekuwa akiangaziwa sana katika kipindi cha miezi kadhaa ambacho kimepita alipakia video ya Mama Sonya kutoka Urusi akiwa amemshika binti yao Sonya Wilsovna huku wakisikiliza wimbo wake 'My Woman'.

Msanii huyo aliyezingirwa na sarakasi tele katika taaluma yake ya muziki aliambatanisha video hiyo na ujumbe maalum akiapa kufanya lolote awezalo ili kumlinda bintiye.

"Binti yangu Sonya na mama yake wanatulia tu. Kama baba, nitafanya kila kitu kumlinda binti yangu" Willy Paul aliandika.

Willy Paul alitangaza kuzaliwa kwa binti yake, Sonya na mwanamitindo huyo wa Kirusi mwishoni mwa mwaka jana.

Sonya ni mtoto wa pili wa  Willy Paul anayejulikana.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 28 ana mtoto mwingine, KingDamian Radido Opondo ambaye alipata na mwanadada wa hapa nchini Kenya anayemtambulisha tu kama Mama Damian.

Willy Paul hata hivyo mara nyingi ameonekana kumpendelea zaidi  baby mama wake Mrusi na inaaminika huenda bado wako katika mahusiano.

Nyota huyo wa muziki wa kisasa alimshirikisha Mama Sonya katika video ya kibao chake cha hivi majuzi 'My Woman' .