(+Video) "Eric wewe ni pumbavu!" Bien na Eric Omondi wakabiliana katika tamasha ya Konshens

Muhtasari

•Bien na Omondi ambao walikuwa wameandamana na walinzi wao walitofautiana kuhusu suala la wasanii wa Kenya kufungulia wasanii wa kigeni jukwaa wanapokuja kutumbuiza hapa nchini.

Eric Omondi, Bien
Eric Omondi, Bien
Image: INSTAGRAM

Usiku wa Ijumaa Wakenya waliohudhuria tamasha kubwa  ya staa wa Dancehall Konshens walipata burudani ya muziki na ya makabiliano makali kati ya mchekeshaji Eric Omondi na mwanamuziki Bien wa auti Sol.

Wasanii hao wawili ambao wamekuwa kwenye sekta ya burudani kwa miaka mingi hawakusalimiana vizuri walipopatana katika uwanja wa Carnivore ila badala yake walianza kukeleleshana na kutupiana maneno makali.

Bien na Omondi ambao walikuwa wameandamana na walinzi wao walitofautiana kuhusu suala la wasanii wa Kenya kufungulia wasanii wa kigeni jukwaa wanapokuja kutumbuiza hapa nchini.

Bien alimkosoa Eric kwa kuendelea kulalamikia hilo huku akimuarifu kuwa haijalishi anayeimba wa mwisho ila cha muhimu zaidi ni pesa ambazo msanii atatia mfukoni tamasha ikitamatika.

"Kila siku uko kwa blogs ukiongea matako, ongea saa hii. Eric wewe ni mjinga! Haijalishi atakayetumbuiza wa mwisho, nimelipwa pesa nyingi kuwa hapa. Nimelipwa pesa zangu mimi!" Bien alisikika akimwambia Omondi.

Omondi alimueleza Bien kwamba ajenda anayoisukuma `itakuwa ya manufaa kwa wasanii wa kizazi kipya, jambo ambalo mwanabendi huyo wa Sauti Sol hakukubaliana nalo.

Bien alimtahadharisha mchekeshaji huyo dhidi ya kuendeleza ajenda yake huku akimwagiza ajipiganie mwenyewe.

"Cha muhimu ni walipwe wafanye kazi yao. Wanalipwa. Niko na Nvirii na Bensol na wanalipwa, wewe ndio mjinga. Enda ujipiganie mwenyewe,!" Bien alisema.

Bien pia  alidhihaki mtindo wa mavazi wa mchekeshaji huyo  na vilevile mtindo wake wa nywele.