"Usiwahi kujali watu wanasema nini!" Carrol Sonnie aandikiwa ujumbe maalum na babake

Muhtasari

•Bw Njoro amesema anajivunia sana kuwa baba ya Sonnie huku akimhakikishia upendo mkubwa ambao anao kwake pamoja na ndugu zake.

•Bw Njoro hakusahau kupatia binti yake ushauri katika ujumbe wake huku akimsihi asiangazie maneno ya watu ila aendelee kukimbilia ndoto zake.

Image: INSTAGRAM// CARROL SONNIE

Siku ya leo (Januari 6)  mwigizaji Caroline Muthoni almaarufu kama Carrol Sonnie anaadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Wanamitandao wa tabaka mbalimbali, familia na marafiki wameendelea kumwandikia mpenzi huyo wa zamani wa Mulamwah jumbe tamu za kheri za kuzaliwa mnamo siku hii maalum maishani mwake.

Mmoja wa ambao wamemsherehekea malkia huyo kwa ujumbe maalum ni baba yake ambaye anajitambulisha kama Njoro Sam kwenye mtandao wa Facebook.

Katika ujumbe wake, Bw Njoro amesema anajivunia sana kuwa baba ya Sonnie huku akimhakikishia upendo mkubwa ambao anao kwake pamoja na ndugu zake.

"Miaka kadhaa nyuma ulinifanya kuwa baba. Ninapotazama nyuma katika safari hiyo namshukuru Mungu tu kwa zawadi ya wewe kuwa binti yangu. Unaposherehekea siku yako ya kuzaliwa leo naomba nithamini upendo wangu kwako na kwa wadogo zako" Bw Njoro aliandikia binti yake Muthoni.

Bw Njoro hakusahau kupatia binti yake ushauri katika ujumbe wake huku akimsihi asiangazie maneno ya watu ila aendelee kukimbilia ndoto zake.

"Maisha haya yanategemea jinsi unavyoyachukua. Ukiichukua vyema itatoa matokeo mazuri. Kwa hivyo nakuambia uwe na umakini na usijali kamwe watu wanasema nini. Wewe ni mkimbiza ndoto. Kuwa na maadhimisho mema ya siku ya kuzaliwa  na afya yako na mali zikupate. Heri ya kuzaliwa Carol Sonnie" Bw Njoro aliandika.

Ujumbe wa Bw Njoro unajiri takriban mwezi mmoja baada ya binti yake kutengana na baba ya binti yake,  mchekeshaji David Oyando almaarufu kama Mulamwah.

Suala hili lilizua gumzo kubwa haswa mitandaoni ya kijamii huku wengi wakitaka kuelewa mbona wakaafikiana kutengana miezi michache tu baada ya kubarikiwa na mtoto wao wa kwanza. Majibu bado hayajapatikana kufikia sasa.