"Gurudumu halikuwa linazunguka vizuri" Mulamwah afunguka kuhusu kutengana kwake na Sonnie

Muhtasari

•Mulamwah alifichua kwamba mojawapo ya sababu zilizomfanya kuamua kuondoka ni mpenziwe kudai angetaka kuishi vizuri zaidi ilhali yeye bado hakuwa sawa kifedha.

•Mulamwah aliweka wazi kwamba kwa sasa hakuna ugomvi wowote kati yao huku akifichua kuwa bado huwa wanawasiliana ingawa sio mara nyingi.

Image: INSTAGRAM// MULAMWAH

Mchekeshaji mashuhuri David Oyando almaarufu kama Mulamwah  amefunguka kuhusu kutengana kwake  na aliyekuwa mpenzi wake Carrol Sonnie. 

Akiwa kwenye mahojiano na Mseto, Mulamwah alikiri kwamba waliafikia makubaliano ya kusitisha mahusiano yao hata kabla ya mtoto wao kuzaliwa, wakati aliyekuwa mpenzi wake alikuwa na ujauzito wa miezi mitatu.

Mulamwah alifichua kwamba mojawapo ya sababu zilizomfanya kuamua kuondoka ni mpenziwe kudai angetaka kuishi vizuri zaidi ilhali yeye bado hakuwa sawa kifedha.

"Niliachwa kwanza, nikarudiwa  alafu pia mimi nikaona niondoke. Niliachwa nikajaribu kufuatilia maneno nikaona bado ni magumu kidogo. Wakati huo yeye alikuwa ameanza kusema anataka kukaa poa na mimi siko sawa kwa hivyo nikaondoka" Mulamwah alieleza.

Mchekeshaji huyo alisema kulikuwa na sababu zingine nyingi zilizosababisha kutengana kwao. Hata hivyo alieleza kwamba waliamua kusalia kimya kuhusu yaliyotokea ili kulinda familia zao.

Mulamwah aliweka wazi kuwa kwa sasa hakuna ugomvi wowote kati yao huku akifichua kwamba  bado huwa wanawasiliana ingawa sio mara nyingi.

"Mimi ni kijana mwenye akili zangu. Siwezi kusema nilichanganywa na mtu ili nitoke kwa mahusiano hayo. Ni kuelewana tu tunaambiana hii kitu haifanyi kazi , mi nakutakia mazuri, nitakuunga mkono hapa na pale. Huwa tunazungumza, huwa namsaidia, huwa nafanya mengi. Bado nasimamia Carrol Sonnie, bado nasimamia mtoto, huwa nawafanyia dili. Hakuna kukosana. Ni ile tu gurudumu halikuwa linazunguka vizuri  katika maisha. Huwa tunazungumza lakini sio kwa sana. Labda iwe  kitu cha maana kati yetu"  Alisema.

Mchekeshaji huyo alieleza kwamba licha ya kuwa walitengana na Sonnie kabla ya mtoto wao  kuzaliwa aliamua kumsaidia katika safari yake ya ujauzito kwani alielewa fika kuwa mama anafaa kulindwa vizuri hadi ajifungue.