Mulamwah ataja mambo ambayo alipenda zaidi kuhusu aliyekuwa mpenziwe Carrol Sonnie

Muhtasari

•Mchekeshaji huyo alisema mpenzi huyo wake wa zamani hakuwa mwenye kuchagua sana na alitosheka na kidogo kilichopatikana.

• Alifichua kwamba walipokuwa kwenye mahusiano Carrol Sonnie angefanya juhudi za kutafuta kile walichohitaji wakati yeye mwenyewe alishindwa.

Image: INSTAGRAM// MULAMWAH

Mchekeshaji David Oyando almaarufu kama Mulamwah amefunguka kuhusu mahusiano yake ya hapo awali na aliyekuwa mpenzi wake Carrol Sonnie.

Akiwa kwenye mahojiano na Mseto East Africa, Mulamwah alikiri kuwa atamkumbuka Sonnie zaidi kwa unyenyekevu na uchangamfu wake.

Mchekeshaji huyo alisema mpenzi huyo wake wa zamani hakuwa mwenye kuchagua sana na alitosheka na kidogo kilichopatikana.

"Sonnie huwa amechangamka, ni mtu  ambaye anaweza kubadili tabia mara moja. Kitu ikitokea tunahitaji kufanya, anaingia haraka.Yeye ni mnyenyekevu sana. Zaidi yake kuwa ni mrembo, yeye ni mnyenyekevu. Ile maharage mtakula, ile nyumba ndogo mtakaa, hachagui" Mulamwah alisema.

Mulamwah alimshauri mama huyo wa binti yake kuendelea kuwa mnyenyekevu hata katika mahusiano yake mengine huku akimuonya dhidi ya kupata tamaa kubwa anapoendelea kupata umaarufu zaidi.

Amemshauri kuwa na subira huku akimweleza kwamba mambo mazuri huhitaji muda ili kutimia.

"Ningeomba sana aendelee kukaa hivo. Hata kwa mahusiano yake mengine aendelee tu na unyenyekevu huo. Utapata wakati anaendelea na usanii na anapata umaarufu zaidi, vitu vitamchanganya anaanza kutamani hiki na kile, anaanza kukaa na yule na yule. Unapata  vitu vinaanza kuharibika. Ningependa ahifadhi unyenyekevu na apatiane  muda. Hizi vitu zote ni muda tu ndio bado" Mulamwah alisema.

Mchekeshaji huyo pia  alifichua kwamba walipokuwa kwenye mahusiano Carrol Sonnie angefanya juhudi za kutafuta kile walichohitaji wakati yeye mwenyewe alishindwa.

"Kuna wakati ambapo singeweza kununua hiki na kile. Kuna wakati ambapo singeweza kumpeleka mahali fulani, labda kuna nguo fulani Mulamwah hangeweza kununua. Yeye angeenda aitafute mahali fulani kwa  jamaa fulani. Unapata unafurahia sana" Alisema.

Baba huyo wa mtoto mmoja ameshauri wanadada kuwa na subira na wapenzi wao na kuacha tamaa ya kupata vitu kwa haraka.