"Tafadhali mtusaidie!" Familia ya Akuku Danger kuandaa hafla ya kuchangisha pesa za hospitali

Muhtasari

• Silprosa alitangaza kwamba Akuku Danger ameweza kuhamishwa kutoka HDU na kupelekwa katika wodi ya kawaida.

•Amesihi Wakenya kuendelea kutoa mchango bila kuchoka kwani kiasi cha pesa kilichopatikana kufikia sasa bado hakijatosha.

Image: INSTAGRAM/ SANDRA DACHA

Hatimaye hali ya afya ya mchekeshaji wa Churchill Show, Akuku Danger imeweza kuimarika na hayuko tena katika hatari kubwa.

Siku ya Jumanne mwandani wake Sandra Dacha almaarufu kama Silprosa alitangaza kwamba ameweza kuhamishwa kutoka HDU na kupelekwa katika wodi ya kawaida.

Hata hivyo Silprosa alisema bili ya hospitali ya Akuku Danger imeendelea kupanda juu kwa kasi kubwa na kufichua kwamba kwa sasa imefikia Sh2.6M. Alisema ingawa tayari wameweza kulipa Sh1.2M, bili hiyo inatarajiwa kupanda hadi wakati mchekeshaji huyo atakapopewa ruhusa kuenda nyumbani.

"Habari njema ni kuwa Akuku Danger sasa amehamishiwa kupelekwa wodi ya kawaida. Bili ya hospitali ni 2.6M lakini tumeweza kulipa 1.2M. Kwa hivyo tuna salio la 1.4M na bili hii sio ya mwisho na unaweza kubadilika hadi Akuku atolewe" Silprosa alisema.

Mwigizaji huyo wa Auntie Boss pia ametangaza kwamba familia inapanga hafla ya kuchangisha pesa  zaidi za matibabu kwa kuwa wameishiwa na uwezo.

Amesihi Wakenya kuendelea kutoa mchango bila kuchoka kwani kiasi cha pesa kilichopatikana kufikia sasa bado hakijatosha.

"Tunapanga hafla ya kuchanga pesa kwa dharura kwa sababu hatuna pesa kwa sasa. Tafadhali aki mtusaidie. Msichoke kutuma hata kama mlishatuma. Unaweza kutuma tena na tena. Mungu awabariki nyote. Nambari ya malipo - 891300 Jina la akaunti- Akuku" Silprosa aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Dacha aliambatanisha ujumbe wake na video iliyoonyesha akimhudumia Akuku Danger na kuwasiliana naye.