Ringtone Apoko azungumza kuhusu maendeleo ya afya yake kufuatia shambulio la Alai la rungu

Muhtasari

•Apoko alisema amekuwa akihisi kizunguzungu na hata kuzimia wakati mwingine kutokana na kugongwa kichwani.

•Amesema kwamba madaktari wamependekeza afanyiwe upasuaji ili kukagua hali ya mfupa wake wa mkono huku akidai kuwa fimbo ya Alai ilisababisha athari kubwa wakati ilipomgonga

Image: INSTAGRAM// RINGTONE APOKO

Mwanamuzki wa nyimbo za injili Ringtone Apoko amesisitiza kuwa bado hajapata afueni kikamilifu kufuatia shambulio la rungu la mwanablogu Robert Alai ambalo lilitokea mwaka jana.

Akiwa kwenye mahojiano na Mpasho, mwanamuziki huyo alidai kwamba angali anakabiliwa na athari za shambulio hilo lililotokea katika barabara moja jijini Nairobi baada ya wawili hao kutofautiana.

Apoko alisema amekuwa akihisi kizunguzungu na hata kuzimia wakati mwingine kutokana na kugongwa kichwani. 

"Mkono imepona. Lakini huwa nahisi baridi wakati mwingine. Huwa  nahisi mfupa inauma wakati wa baridi. Wakati mwingine huwa nahisi kizunguzungu, kuna wakati huwa naishiwa na nguvu na kuanguka chini kwa  sababu ya kichwa. Nimekuwa nikifaint ni vile tu naogopa kupost kwa sababu watu watasema  eti najifanya" Apoko alisema.

Mwanamuziki huyo amesema kwamba tayari ameomba ushauri wa daktari katika juhudi za kusuluhisha matatizo yake ya kiafya.

Amesema kwamba madaktari wamependekeza afanyiwe upasuaji kukagua hali ya mfupa wake wa mkono huku akidai kwamba fimbo ya Alai ilimsababisha athari kubwa.

"Wakati mwingine huwa naumwa sana. Hata nimeomba ushauri wa daktari wangu akaniambia itabidi nifanyiwe upasuaji ili waweze kuangalia kama mfupa  wangu ulipasuka. Huwa nashindwa kubeba vitu. Ili rungu niligongwa ilikuwa ngumu sana" Apoko alisema.

Msanii huyo aliyezingirwa na drama si haba katika taaluma yake amewasuta wale ambao wamekuwa wakitilia shaka maumivu yake huku akisisitiza kwamba angali anaumia.