"Ningependa kuzeeka pamoja nawe!" Terence Creative amsherehekea mkewe Milly Chebby

Muhtasari

•Mchekeshaji huyo amemhakikishia mkewe kuhusu mapenzi makubwa aliyonayo kwake huku akimwambia angependa kuwa naye hadi miaka ya uzeeni.

Image: INSTAGRAM// MILLY CHEBBY

Hivi leo (Januari 18) mwanavlogu mashuhuri Millicent Chebet almaarufu kama Milly Chebby anaadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Mke huyo wa mchekeshaji Lawrence Macharia almaarufu kama Terence Creative anasherehekea kuhitimu miaka 35.

Chebby amemshukuru Maulana kwa kuendelea kumlinda huku akieleza imani yake kwamba ana mipango mikubwa juu ya maisha yake.

"Leo ninaongeza mwaka mmoja zaidi. Ninashangaa  jinsi Mungu amekuwa mwaminifu katika maisha yangu. Mungu umenilinda kama mboni ya jicho lako, umenificha chini ya kivuli cha mabawa yako. Nakushukuru milele Mungu. Najua Mungu una mipango mikubwa zaidi kwangu mwaka huu unaokuja . Heri ya siku ya kuzaliwa ya 35 kwangu" Chebby  ameandika kwenye ukurasa  wake  wa  Instagram.

Mamia ya wanamitandao ikiwemo watu mashuhuri wameendelea kumtakia malkia huyo heri njema za siku ya kuzaliwa.

Terence Creative hajachelewa kuandikia kipenzi chake ujumbe mtamu anapopiga hatua nyingine maishani.

Mchekeshaji huyo amemhakikishia mkewe kuhusu mapenzi makubwa aliyonayo kwake huku akimwambia angependa kuwa naye hadi miaka ya uzeeni.

"Siku zote natamani kuzeeka na wewe mpenzi, nataka kuamkia tabasamu lako la kupendeza hata nikiwa na umri wa miaka 99. Unapoongeza mwaka mmoja, sikutakii kingine ila bora zaidi, Mungu akutimizie mahitaji yote ya maisha yako. Upate neema na utukufu zaidi waMungu. Nakupenda na sababu mpenzi wangu  Milly Chebby. Heri za kuzaliwa mpenzi wangu"  Terence amemwandikia Milly.

Wanandoa hao wamekuwa pamoja kwa muda mrefu na kufikia sasa wamebarikiwa na mtoto mmoja.