The Wajesus waweka bango kubwa barabarani kutangazia ulimwengu ujauzito wa mtoto wao wa pili

Muhtasari

•Wanavlogu hao walishangaza dunia kwa kutangaza habari njema zisizotarajiwa kuhusu ujauzito wa mtoto wao wa pili.

•Kabi alieleza kwamba iligharimu takriban shilingi milioni moja unusu kufanya matangazo ya ujauzito huo.

Image: INSTAGRAM// MILLY WAJESUS

Siku ya Jumanne ilikuwa siku maalum kwa wanandoa mashuhuri Peter Kabi na Millicent Wambui wa The Wajesus Family pamoja na maelfu ya mashabiki wao.

Wanavlogu hao walishangaza dunia kwa kutangaza habari njema zisizotarajiwa kuhusu ujauzito wa mtoto wao wa pili.

Wawili hao walitumia kurasa zao za mitandao ya kijamii, wanahabari wa mitandaoni pamoja na akaunti yao ya YouTube kufahamisha mashabiki wao kuhusu baraka hiyo iliyowapa kuelekea mwishoni mwa mwaka jana.

"Tunayo furaha kubwa hatimaye kutangazia familia yetu ya mtandaoni habari za kusisimua. Familia ya Wajesus inaendelea kukua na tunampa Mungu utukufu wote. Ametuchagua kuwa wazazi kwa mara nyingine tena na kuunganisha pamoja mtoto ili ajiunge na familia yetu" Milly alitangaza kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Isitoshe, Kabi aliamua kushangaza mpenzi wake kwa kuweka tangazo hilo kwenye ubao mkubwa wa matangazo ambao uliwekwa kando ya barabara ya Limuru, jijini Nairobi.

Kabi alishirikiana na kampuni moja ya mavazi ya watoto ya hapa nchini kufanya tangazo hilo.

Walipokuwa wanazungumza na wanahabari baada ya kutangazia ulimwengu habari hizo nzuri, wanandoa hao walisema bango hilo litasalia pale kwa kipindi cha angalau miezi miwili.

Kabi alieleza kwamba iligharimu takriban shilingi milioni moja unusu kufanya matangazo ya ujauzito huo. Alisema alishirikiana na wadau wengine kufanya matangazo hayo.

Mtoto atakayezaliwa atakuwa wa tatu wa Kabi na wa pili wa mpenzi wake Milly.

Mwaka wa 2020, Milly Wajesus aliweka bango kubwa barabarani kusherehekea siku ya kuzaliwa ya mpenzi wake Kabi.