Rufftone kuwania useneta wa Nairobi kwa UDA

Muhtasari

• Amezungumza mengi kuhusu azma yake na sababu kuu kuingia mrengo wa naibu Rais William Ruto na si ODM kama wengi wa wafuasi wake walivyokuwa wakitarajia.

• Ruffton anafahamika sana kwa wimbo wa injili kwa jina 'Mungu Baba', kibao ambacho aliwashirikisha polisi kutoka kitengo cha GSU takribani miaka minane iliyopita.

RUFFTONE
RUFFTONE
Image: HISANI

Mwanamuziki wa injili Smith Mwatia almaarufu Ruffton na ambaye ana azma ya kuwa seneta wa Nairobi ametangaza kwamba atagombea kiti hicho kwa tiketi ya UDA.

Amezungumza mengi kuhusu azma yake na sababu kuu kuingia mrengo wa naibu Rais William Ruto na si ODM kama wengi wa wafuasi wake walivyokuwa wakitarajia.

Ruffton anafahamika sana kwa wimbo wa injili kwa jina 'Mungu Baba', kibao ambacho aliwashirikisha polisi kutoka kitengo cha GSU takribani miaka minane iliyopita.

Mwanamuziki huyo anadai kuwa uamuzi wake kujiunga na mrengo wa naibu rais unatokana na madai kuwa chama cha ODM kinahusishwa pakubwa na wahuni wapenda vurugu na ndio sababu kuu imemfanya kuingia UDA.

Akitoa mfano, Ruffton alisema mwaka 2007 baada ya uchaguzi mkuu, ndugu yake Daddy Owen, ambaye pia ni mwanamuziki tajika wa nyimbo za injili alimfurusha nyumbani kwa upanga,  baada ya kutofautiana vikali kuhusu siasa za mirengo pinzani wakati huo.

Ruffton anasema kipindi hicho yeye alikuwa mfuasi wa chama cha PNU ambacho ni cha  rais mstaafu Mwai Kibaki ilhali ndugu yake Daddy Owen alikuwa ni mfuasi sugu wa chama cha ODM.

Kisa hicho cha Owen kumfukuza Ruffton kwa panga kilimpelekea kuchukia chama cha ODM na hata kukihusisha na vurugu za uchaguzi.