"Nimechoka!" Pritty Vishy atangaza kutengana na mwanamuziki Stivo Simple Boy

Muhtasari

•Vishy amesema amechoshwa kabisa na mvurutano uliopo kwenye mahusiano yao na kwa sasa angependa kupata utulivu wa mawazo.

•Ameeleza kwamba hakupendezwa na jinsi mwanamuziki huyo alishindwa kujisimamia na jinsi alishawishiwa virahisi na watu wengine.

Pritty Vishy na Stivo Simple Boy
Pritty Vishy na Stivo Simple Boy
Image: HISANI

Mwanadada anayejitambulisha kama mpenzi wa mwanamuziki Stivo Simple Boy, Purity Vishenwa almaarufu kama Pritty Vishy ametangaza kwamba ako tayari kusonga mbele na maisha yake kivyake.

Akiwa kwenye mahojiano na Mzuka Kibao Tv, Vishy alikiri hakujakuwa na uhusiano mwema kati yake na Simple Boy kwa muda sasa na kufichua kwamba msanii huyo hata hajakuwa akipokea simu zake licha ya juhudi zote alizofanya kumfikia.

Vishy amesema amechoshwa kabisa na mvurutano uliopo kwenye mahusiano yao huku akimuombea mwanamuziki huyo mema katika hatua zake zijazo.

"Nimechoka! Nimechoshwa na maskendo,nimechokeshwa na yeye, nimechoshwa na usimamizi wake. Nataka tu kupata utulivu wa akili. Stivo Simple Boy nina furaha juu yako. Shukran kwa muda ambao tumekuwa pamoja. Nakuombea sana upate mtu atakayekupenda jinsi ulivyo" Vishy alisema.

Mwanadada huyo alifichua kwamba walianza kuchumbiana na Simple Boy mnamo mwaka wa 2019 baada ya kuwa marafiki kwa muda.

Hata hivyo alieleza kwamba hakupendezwa na jinsi mwanamuziki huyo alishindwa kujisimamia na jinsi alishawishiwa virahisi na watu wengine.

"Labda kuna mtu anayenifaa huko nje na naendelea kujisukuma pale. Labda yeye ako na mtu mwenye  atakuja kumfungua akili haraka kuliko  vile nilivyojaribu na najaribu kuzuia. Wacha aende huko nje ajaribu nami nijaribu" Alisema.

Hivi majuzi Simple Boy aliweka wazi kwamba hakuna mahusiano yoyote kwa sasa kati yake na Pritty Vishy.

Vishy amesema hana shida yoyote iwapo huo ndio uamuzi ambao mwanamuziki huyo ameafikia huku akiapa kutomsamehe hata akijuta.