King Kaka afichua alikuwa amepatiwa mwezi mmoja wa kuishi alipokuwa anaugua mwaka jana

Muhtasari

•Madaktari walimwarifu kuwa amesalia na mwezi mmoja wa kuishi baada ya kugunduliwa kuwa na mashimo kwenye mapafu yake.

•Wanamitandao wameendelea kusherehekea afueni ya mwanamuziki huyo na kumtakia maisha marefu.

Image: INSTAGRAM// KING KAKA

Mwanamuziki wa nyimbo za kufoka Kennedy Ombima almaarufu kama King Kaka amefunguka zaidi kuhusu maradhi yaliyokuwa yanamwathiri kwa kipindi cha zaidi ya miezi mitatu mwaka jana.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, King Kaka amefichua kwamba alipokuwa anaugua madaktari waliwahi kumwarifu kuwa amesalia na mwezi mmoja wa kuishi baada ya kugunduliwa kuwa na mashimo kwenye mapafu yake.

Rapa huyo amejivunia kuona kwamba miezi minne baadae yu buheri wa afya. Hata hivyo amefichua kuwa mashimo mawili ambayo aligunduliwa kuwa nayo kwenye mapafu bado yako.

"Xray yaonyesha niko na mashimo kwa mapafu yangu bado. Walinipa 30 days niishi, hiyo ilikuwa miezi mitatu iliyopita" King Kaka alisema.

Mwaka jana mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 34 alilazwa hospitalini kwa kipindi kirefu baada ya afya yake kudhoofika kufuatia vipimo vibaya vya daktari.

Ugonjwa uliokuwa umemwathiri King Kaka ulimfanya apoteze hisia ya ladha, hamu ya chakula, uzito wa mwili kati ya dalili zingine za kutisha.

Wanamitandao wameendelea kusherehekea afueni ya mwanamuziki huyo na kumtakia maisha marefu.

@taliaoyando Umeandikiwa ukuu.. Mungu ni mwema

@daddyowen Rafiki yangu, Nakuombea ufurahie afya njema na yote yakwendee vyema  hata moyo ukiendelea vizuri

@vivannymoney Neema ya Mungu bado unayo mengi ya kufanya hapa duniani na miaka mingi ya kuishi