Usiwahi omba msamaha kwa kuzaliwa katika familia tajiri- Akothee amshauri mpenziwe Nelly Oaks

Muhtasari

•Mama huyo wa watoto watano amemshauri Oaks aendelee kutia bidii na ajiinue zaidi huku akimtaja mpenzi huyo wake kama mtu mwenye hekima.

Nelly Oaks na Akothee
Nelly Oaks na Akothee
Image: INSTAGRAM//NELLY OAKS

Mwanamuziki na mjasiriamali  mashuhuri nchini Esther Akoth almaarufu kama Akothee amemshauri mpenzi wake Nelly Oaks kufumbia maskio maneno ya  watu wanaokosoa mtindo wake wa maisha wa kifahari.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Akothee amemsihi Oaks kutoogopa kujigamba na mali yake huku akimweleza kuwa sio hatia yake kwamba alizaliwa katika familia tajiri.

Mama huyo wa watoto watano pia amemshauri Oaks aendelee kutia bidii na ajiinue zaidi huku akimtaja mpenzi huyo wake kama mtu mwenye hekima.

"Usiwahi kuomba msamaha kwa kuzaliwa katika familia tajiri, sio kosa lako! Kosa lako litakuwa iwapo hutachukua sahani hiyo ya fedha na kujiinua hadi kiwango hicho kingine! Kuwa bora zaidi kwa ubinafsi wako! Usijisikie mwenye hatia kwa kuonyesha jasho lako, haina uhusiano wowote na asili ya familia yako au urithi , hekima haiwezi kurithiwa," Akothee aliandika.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 42 ameonyesha fahari kubwa kwa mpenzi wake na maendeleo wanayofanya pamoja ikiwemo ujenzi wa nyumba katika kaunti ya Kilifi.

"Mkurugenzi Mtendaji wa Oaks Media endelea kusukuma mpenzi wangu! Anga sio kikomo. Najua uwezo wako, unajua hilo.  Rafiki yangu bora wa wakati wote, mwenzangu kwa udaku, mpenzi wangu na mume wangu wa pekee. Njoo tumalize hizo nyumba za kilifi ili wajue Nelly Oaks ni nani. Ndio waseme nimekula prsa za mtoto MCM wangu," Amesema.

Nelly Oaks kwa upande wake amemshukuru mwanamuziki huyo kwa maneno ya busara aliyompa.