" Ni ushamba!" Huddah Monroe awakashifu wafanyibiashara wanaohujumu watu mashuhuri

Muhtasari

•Huddah amewasihi wafanyibiashara wote kutokuwa wabaguzi na kuwa na bei sawa ya bidhaa zao kwa wateja wote.

•Amewakosoa vikali wauzaji ambao wamekuwa wakimhadaa na kusisitiza kuwa hata kama yeye sio fukara hayuko tayari kutumia hela zake kiholela.

Image: INSTAGRAM// HUDDAH MONROE

Mwanasoshalaiti na mjasiriamali mashuhuri Huddah Monroe ameonyesha ghadhabu dhidi ya wafanyibiashara wanaowatoza watu mashuhuri zaidi ya bei ya kawaida kwa bidhaa zao.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Huddah amewasihi wafanyibiashara wote kutokuwa wabaguzi na kuwa na bei sawa kwa wateja wote.

Kulingana na mwanasoshalaiti huyo, kitendo cha wauzaji kutoza watu mashuhuri ada zaidi kwa bidhaa zao ni ushamba na kinawafanya wapoteze wateja wengi.

"Watu hapa wanafikiri watu mashuhuri si watu wa kawaida. Nikipiga simu ama kutuma ujumbe kuagiza bidhaa nalipishwa mara tatu zaidi. Mwakilishi wangu akipiga simu inakuwa sio ghali. Siku hizi huwa situmi jumbe ama kupiga simu huwa naacha mtu mwingine anifanyie hilo. Nachukia mawazo hayo ya kikale.  Unafaa kushukuru kuwa nataka kutumia huduma zako. Tendeeni watu kwa usawa. Nyote mlipoteza mteja lakini bado naendelea kutumia huduma zenu kwa bei rahisi. Mlinipoteza" Huddah ameandika.

Muuzaji huyo wa vipondozi vya 'Huddah Cosmetics' amesema kuwa mara nyingi anapoenda kununua bidhaa huwa anadaiwa zaidi ya mara ya tatu ya bei ya kawaida.

Amewakosoa vikali wauzaji ambao wamekuwa wakimhadaa na kusisitiza kuwa hata kama yeye sio fukara hayuko tayari kutumia hela zake kiholela.

"Hii ni pesa ya jasho na damu yangu. Haikuji kwa urahisi. Kwa kweli hatutalipa mara tatu ya bei ya kawaida kwa sababu sisi ni mashuhuri na tunaishi maisha ya hadhii ya juu" Amesema Huddah.

Huddah amewashauri wafanyibiashara wote kutupilia mbali dhana ya kutoza watu mashuhuri zaidi huku akisema imepitwa na wakati