Babake Diamond amsifia sana Zuchu, amkubali kuwa mke wa mwanawe

Muhtasari

•Mzee Abdul alimtaja Zuchu kama mwanadada aliyelelewa vizuri na mwenye maadili mema huku akiweka wazi kwamba atafurahi sana iwapo ndoa inayoripotiwa itakuja kutimia.

•Alisema anaamini malkia wa Bongo Zuchu anamfaa mwanawe Diamond, sio kwa sura tu ila pia kwa tabia zake ambazo alizitaja kuwa nzuri.

Mzee Abdul abariki ndoa ya Diamond na Zuchu
Mzee Abdul abariki ndoa ya Diamond na Zuchu
Image: HISANI

Mzee Abdul Juma ameidhinisha ndoa inayozungumziwa sana kati ya mwanawe Diamond Platnumz na Bi Zuhura Othman almaarufu kama Zuchu.

Akiwa kwenye mahojiano ya hivi karibuni na Mbengo TV, Mzee Abdul alisema haoni tatizo lolote kwa Zuchu kuwa mke wa mwanawe.

Babake Diamond alimtaja mtunzi huyo wa kibao 'Sukari' kama mwanadada aliyelelewa vizuri na mwenye maadili mema huku akiweka wazi kwamba atafurahi sana iwapo ndoa inayoripotiwa itakuja kutimia.

"Nitafurahi zaidi. Zuchu ni mwanamke mzuri vilevile, ana uwezo. Isitoshe ametoka sehemu yenye ibada ya suala zote za Uislamu, kafunzwa vizuri. Mamake namwelewa vizuri vilevile, kashauriwa mara nyingi. Anajielewa, ana tabia njema. Sio mtu mbaya," Mzee Abdul alisema.

Mpenzi huyo wa zamani wa Mama Dangote amesema hatua ya Diamond kuoa itakuwa ya baraka sio kwake tu ila kwao kama wazazi wake.

Mzee Abdul alisema anaamini malkia wa Bongo Zuchu anamfaa mwanawe Diamond, sio kwa sura tu ila pia kwa tabia zake ambazo alizitaja kuwa nzuri.

"Zuchu sio mbaya, ni msichana mzuri. Amefunzwa, anaelewa  malengo ya kibinadamu anaelewa utu ni nini, anafaa kwa kila kitu. Ametoka kwa familia bora, ina uongozi bora wa kimaisha. Sio mbaya kusema kweli. Mwanamke mara nyingi inakuwa sio sura. Mwanamke tabia. Naamini Zuchu sio mbaya, kikubwa maelewano. Maisha yaendelee,waangalie ndoa. Mwenyezi Mungu awafungulie kama kweli kuna kitu kama hicho" Mzee Abdul alisema.

Aliendelea kuwekea mkono ndoa inayokadiriwa ila akaeleza anatarajia chochote kwani huenda ikawa kiki kama baadhi ya watu wanavyodai.