•Alisema hana ufahamu wowote kuwa tayari familia na wazee kutoka upande wa Diamond wamekutana na mama yake Khadija Kopa na kuwasilisha posa.
•Zuchu pia alieleza kuwa hina ambayo amepakwa mikononi kwa sasa ni mapambo tu wala sio kumaanisha amechumbiwa.
Malkia wa Bongo Zuhura Othman almaarufu kama Zuchu amekana madai kwamba mipango ya harusi yake na bosi wa WCB Diamond Platmunz iko karibu kukamilika.
Akiwa kwenye mahojiano na Wasafi Media, Zuchu alisema madai kuwa tayari amechumbiwa na kuvalishwa pete na Diamond hayana ukweli wowote.
Mwanamuziki huyo kutokea Zanzibar alisema hana ufahamu wowote kuwa tayari familia na wazee kutoka upande wa Diamond wamekutana na mama yake Khadija Kopa na kuwasilisha posa.
"Halina ukweli! Ningejua. Iweje mimi ndio bibi harusi na sina taarifa?" Alisema.
Mtunzi huyo wa kibao 'sukari' alikuwa anazungumzia madai kwamba mpenzi wa mamake Diamond Uncle Shamte, meneja Ricardo Momo na wazee kadhaa kutoka upande wa Diamond walipeleka barua nyumbani kwa kina Zuchu kama maandalizi ya harusi yake na bosi huyo wa WCB.
Zuchu pia alieleza kuwa hina ambayo amepakwa mikononi kwa sasa ni mapambo tu wala sio kumaanisha amechumbiwa.
"Ni urembo tu. Napenda hina na mpenzi niliye naye anapenda ndio maana nimepaka" Alisema Zuchu.
Zuchu alipuuzilia mbali madai kwamba ziara ya Mombasa ambayo alifanya hivi majuzi pamoja na mama yake ili kwa minajili ya kufahamisha jamaa zao wanaoishi pale kuhusu mipango ya ndoa.
Alisema kwamba tayari ako kwenye mahusiano na mpenzi mwingine na hana mpango wa kufunga ndoa na Diamond ambaye alimtaja kama bosi wake tu.