Zuchu afunguka kuhusu mpenzi wake halisi baada ya kukana mahusiano ya kimapenzi na Diamond Platnumz

Muhtasari

•Zuchu alidhihirisha kuwa amekuwa katika mahusiano na mpenzi huyo wake wa siri kwa kipindi cha takriban miezi minne.

•Alisema kwamba atamtambulisha mpenzi wake hadharani kwa mara ya kwanza mnamo siku ya Valentines atakapokuwa  ameendalia wapendanao shoo kubwa  jijini Dar es Salaam.

Zuchu akana mahusiano ya kimapenzi na Diamond
Zuchu akana mahusiano ya kimapenzi na Diamond
Image: HISANI

Malkia wa Bongo Zuhura Othman almaarufu kama Zuchu amepuuzilia mbali mahusiano na bosi wake katika WCB Diamond Platnumz.

Akiwa kwenye mahojiano na Wasafi Media, Zuchu aliweka wazi kwamba Diamond Platnumz ni bosi wake na hakuna chochote kinachoendelea kati yao.

Staa huyo wa muziki kutokea Zanzibar alisisitiza kwamba kwa sasa tayari ako kwenye mahusiano na mwanamume mwingine ambaye ni mfanyibiashara.

"Mimi sikai kwa Diamond. Kwa kweli nachumbiana na mtu, niko na boyfriend. Ni mtu tu wa kawaida. Ni mrefu kuliko mimi, ni maji ya kunde, ni mfanyibiashara na anafanya mazoezi. Siwezi kuwa na mtu ambaye hafanyi mazoezi, afya ni kila kitu" Zuchu alieleza.

Zuchu alidhihirisha kuwa amekuwa katika mahusiano na mpenzi huyo wake wa siri kwa kipindi cha takriban miezi minne.

Binti huyo wa gwiji wa taarabu Khadija Kopa alifichua kwamba kwa sasa mpenziwe hayuko nchini Tanzania lakini  ameendelea kumbubujikia  mahaba kutoka mahali alipo. Aliweka wazi kwamba mdoli ambaye alipokea hivi majuzi ulitumwa na mpenziwe kutoka nje ya nchi Tanzania.

Alisema kwamba atamtambulisha mpenzi wake hadharani kwa mara ya kwanza mnamo siku ya Valentines atakapokuwa  ameendalia wapendanao shoo kubwa  jijini Dar es Salaam.

"Niko na uhakika nitakuwa na nimpendaye. Kwa hivyo nashauri watu wengine waje na wapenzi wao. Sio lazima wanandoa, unayempenda ata kama ni mamako ama mtoto wako. Hiyo ni siku ya wapendanao" Zuchu alisema.

Mwanamuziki huyo pia alitangaza kuwa mamake Diamond Platnumz, Mama Dangote pamoja na mpenzi wake Uncle Shamte watahudhuria shoo hiyo.