Zari kapata kipenzi kipya? Video zinazomwonyesha akibubujikia jamaa mahaba zaibua gumzo

Muhtasari

•Kwenye video moja Zari anaonekana akimpelekea GK Chopa chakula na kupiga magoti anapomkabidhi, kama ilivyo ada ya wake kutoka Uganda.

Image: INSTAGRAM// GK CHOPA

Video zinazoonyesha mwanasoshalaiti mashuhuri Zari Hassan akijivinjari na mwanamume kwa njia ya kuibua dhana ya mapenzi zimeacha wanamitandao na maswali chungu nzima.

Mpenzi huyo wa zamani wa nyota wa Bongo Diamond Platnumz alionekana kwenye video kadhaa zinazosambazwa mitandaoni akiwa katika hali ya mahuba na jamaa aliyetambulishwa kama GK Chopa.

Kwenye video moja Zari anaonekana akimpelekea GK Chopa chakula na kupiga magoti anapomkabidhi, kama ilivyo ada ya wake kutoka Uganda.

Video nyingine inaonyesha wazaliwa hao wawili wa Uganda wakiwa wamebarizi katika eneo la burudani huku wakisikiliza muziki mtamu wa mapenzi.

Hivi karibuni Zari amekuwa akionekana sana na jamaa huyo ambaye sio mengi yanafahamika kumhusu.

Hivi majuzi mama huyo wa watoto watano alishambuliwa sana mitandaoni baada ya kupakia video wakiwa na jamaa huyo huku ikidaiwa kuwa ana umri mdogo zaidi kumliko.

Zari hata hivyo alijitokeza kukana mahusiano yoyote ya kimapenzi na GK Chopa na kuwataka wambea kukoma kuangazia maisha yake.

“Patia watu wa Afrika mashariki picha, na wataibuka na aya ndefu za maneno ambao wenyewe ndio wanajua. Kufuatilia mambo ya watu kutakuponza na hakuna atakayeshughulika na wewe!” Zari alisema.

Zari amewahi kuwa katika ndoa na mfanyibiashara marehemu Ivan Semwanga na kubarikiwa na watoto watatu naye. Vile vile alikuwa kwenye mahusiano na mwanamuziki Diamond Platnumz ambaye pamoja walipata watoto wawili.