Juma Jux afunguka kuhusu mahusiano yake miaka baada ya kutengana na Vanessa Mdee

Muhtasari

•Jux aliweka wazi kuwa kwa sasa anafurahia maisha yake na hana kinyongo chochote dhidi ya mpenzi wake wa zamani Mdee.

•Mwanamuziki huyo alisema kuwa anasherehekea mafanikio ya Mdee ya kupata mtoto na mpenzi wake wa sasa Rotimi.

Juma Jux azungumzia madai ya tatizo la uzazi
Juma Jux azungumzia madai ya tatizo la uzazi
Image: HISANI

Staa wa Bongo Juma Mussa Mkambala almaarufu kama Jux amefichua kuwa tayari moyo wake ushatekwa tena na kwa sasa yuko kwenye mahusiano mengine.

Akiwa kwenye mahojiano na Wasafi Media, kigogo huyo wa muziki wa mapenzi alikiri kwamba tayari ashasonga mbele na maisha yake baada ya kutengana na aliyekuwa mpenzi wake Vanessa Mdee.

Jux aliweka wazi kuwa kwa sasa anafurahia maisha yake na hana kinyongo chochote dhidi ya mpenzi wake wa zamani Mdee.

"Mimi nimeshaendelea na maisha yangu, nina raha. Niko kwenye mahusiano mengine" Jux alisema.

Mwanamuziki huyo alisema kuwa anasherehekea mafanikio ya Mdee ya kupata mtoto na mpenzi wake wa sasa Rotimi.

Alipuuzilia mbali madai kwamba alishindwa kumpachika malkia huyo ujauzito kwa kuwa hana uwezo wa kuzalisha mwanamke. Jux alisema sababu iliyowafanya wasipate mtoto walipokuwa kwenye mahusaino ni kwa kuwa hawakuwa tayari

"Kila kitu huwa na mpango. Ule muda ambao tulikuwa pamoja ulikuwa muda ambao mimi na yeye tulikuwa hatuko tayari kuwa hivo. Kuzaa na mtu yeyote wa nje ni maamuzi, sio mabaya. Labda ilifikia muda kwenye mahusiano akawa sasa anataka. Ule muda ambao alikuwa anataka basi akawa hayuko na mimi. Mimi pia nina mipango yangu ya maisha. Siwezi kuzaa mtoto kwa sababu watu wanasema niwe na mtoto" Jux alisema. 

Jux na Vanessa walitengana takriban miaka mitano iliyopita baada ya kuwa kwenye mahusiano kwa kipindi kirefu.

Takriban miaka miwili iliyopita Vanessa alipenda tena na kujitosa kwenye mahusiano na mwigizaji Rotimi ambaye pamoja walibarikiwa na mtoto mwaka uliopita.

Jux amekiri kwamba  hakuwahi pata mtoto na mpenzi wake wa zamani yeyote .