"Niko single!" Kinuthia wa TikTok afunguka kuhusu mahusiano yake

Muhtasari

•Kinuthia ambaye alipata umaarufu mkubwa mwaka uliopita baada ya kudaiwa kujifanya mwanadada na  'Kula fare'  ya shilingi laki tatu ameweka wazi kwamba kwa sasa hachumbiani na mwanamke wala mwanaume yeyote.

Kelvin Kinuthia afunguka kuhusu mahusiano yake
Kelvin Kinuthia afunguka kuhusu mahusiano yake
Image: TWITTER

Mwanavlogu mashuhuri wa TikTok Kelvin Kinuthia amekiri kwamba hana mpenzi wa kusherehekea  naye siku ya wapendanao ya Valentines.

Akiwa kwenye mahojiano na Eve Mungai, Kinuthia ambaye alipata umaarufu mkubwa mwaka uliopita baada ya kudaiwa kujifanya mwanadada na  'Kula fare'  ya shilingi laki tatu aliweka wazi kwamba kwa sasa hachumbiani na mwanamke wala mwanaume yeyote.

"Sina mtu wa kuniletea maua siku ya Valentines. Niko single!" Kinuthia alisema.

Kinuthia alipuuzilia mbali uvumi kuwa anachumbiana na mwanavlogu mwenzake,Tokyo ambaye mara kwa mara wamekuwa wakifanya video pamoja na kuzua maswali mengi miongoni mwa mashabiki.

Mwanablogu huyo amewataka mashabiki wake kutobashiri kuhusu ujinsia na mahusiano yake huku akiwahakikishia kuwa hatimaye atajitokeza na kuweka kila kitu bayana wakati atakapojisikia tayari.

"Watu waache kujijazia. Mngoje mpaka ile siku atajitokeza awaambie" Kinuthia alisema.

Kinuthia alisema mtindo wake wa kuvaa mavazi ya kike na kujipaka vipondozi ni kwa minajili ya kutengeneza video zake na haimaanishi kuwa hayo ni maisha yake ya kawaida.

Aliweka wazi kuwa huwa anavalia mavazi ya kiume anapokuwa katika mazingira yake ya kawaida mbali na kutumbuiza.