'Niliteseka sana!' Justina Syokau afunguka kuhusu sababu zake kugura ndoa miaka tisa iliyopita

Muhtasari

• Alidai kuwa aliyekuwa mumewe hakuwa mwajibikaji na licha yake kuwa mwenye uwezo, hakuwa anashughulikia mahitaji yake ya kifedha.

•Alifichua kwamba ndoa yake ilikumbwa na misukosuko mingi na mumewe angemchapa mara kwa mara bila sababu sahihi.

Mwanamuziki mashuhuri  wa nyimbo za injili Justina Syokau almaarufu kama 'twedi twedi' amedokeza kuhusu sababu zake kugura ndoa miaka tisa iliyopita.

Akiwa kwenye mahojiano na Eve Mungai, mwanamuziki huyo ambaye alipata umaarufu mkubwa miaka miwili iliyopita baada ya kuachilia kibao '2020' alieleza kwamba aliteseka sana wakati alipokuwa kwenye ndoa na baba kwa mtoto wake.

Syokau alidai kuwa aliyekuwa mumewe hakuwa mwajibikaji na licha yake kuwa mwenye uwezo, hakuwa anashughulikia mahitaji yake ya kifedha. Vile vile alimshutumu kwa kupenda wanawake sana.

"Yule jamaa alikuwa anaacha 20bob, na anafanya kazi. Ni mtu ambaye naheshimu. Ni mtu anayeheshimiwa sana hapa Kenya. Yule mwanaume alikuwa womanizer, Najuta kuolewa na mwanaume mpenda wanawake, sikujua. Sikuona tahadhari na hakuwa anawajibika" Syokau alisimulia.

Syokau alifichua kwamba ndoa yake ilikumbwa na misukosuko mingi na mumewe angemchapa mara kwa mara bila sababu sahihi.

Alisema kuwa mumewe alimfanya aache kazi nzuri ambayo alikuwa anafanya na kumpeleka kwao nyumbani, jambo ambalo lilimvuta nyuma kimaisha.

"Najuta kuolewa na mwanaume mpenda wanawake, sikujua. Sikuona tahadhari na hakuwa anawajibika. Niliteseka sana kwa ndoa yangu, nilikuwa nachapwa sana. Tena alinitoa kazi nikawa naenda kuchotea watu maji kule nyumbani kwao. Nilikuwa nafanya kazi katika hospitali ya Kijabe. Alinikuta nikiimba, nilirudi nyumba hata singeweza enda kuimba kwa sababu ndoa ilikumbwa na misukosuko mingi" Syokau alisema.

Mwanamuziki huyo amewatahadharisha wanaume dhidi ya kuwapiga wake zao huku akiwafahamisha kuwa jambo hilo huwa na athari mbaya kwa masuala ya kitandani.

Vilevile amewataka wanawake wanaoteswa na waume zao kuacha kuvumilia na wagure kabla ya mambo kuharibika zaidi.