Mulamwah afunguka kuhusu jinsi hali ya kuwa baba ilibadilisha maisha yake

Muhtasari

• Amesema majukumu mapya yaliyompata yalimfanya aache kufanya mambo bila mpangilio kwani alifahamu kuwa ana familia ya kukimu mahitaji yake.

• Amefichua kwamba licha ya kuwa alitengana na  baby mama wake, bado huwa anapata nafasi ya kumuona bintiye mara kwa mara.

Image: INSTAGRAM// MULAMWAH

Mchekeshaji David Oyando almaarufu kama Mulamwah alijitosa kwenye ulimwengu mpya wa uzazi mnamo Septemba 20 mwaka jana ambapo alikaribisha mtoto wake wa kwanza.

Mulamwah na aliyekuwa mpenzi wake mwigizaji Carrol Sonnie walibarikiwa na mtoto mrembo wa kike na kumpa jina Keilah Oyando.

Mchekeshaji huyo amekiri kuwa hali mpya ya kuwa baba ilibadilisha maisha yake sana hasa kwa upande wa matumizi ya pesa. Amesema majukumu mapya yaliyompata yalimfanya aache kufanya mambo bila mpangilio kwani alifahamu kuwa ana familia ya kukimu mahitaji yake.

"Niliacha tabia kama za kutumia pesa kiholela, kwa mfano kuamka tu na kuenda kupiga sherehe kabisa juu najua nitafanya shoo na nipate zingine. Sasa lazima niwe na mpango. Lazima niwe na maono ya siku zijazo. Huyo mtoto anakua, atataka shule, lazima awe na bima ya afya. Imenibadilisha sana na ni kitu kizuri sana," Mulamwah alisema akiwa kwenye mahojiano na Dr Ofweneke.

Mchekeshaji huyo ambaye pia ni muuguzi alieleza kuwa anafurahia hali hiyo mpya ya kuwa baba na majukumu yanayoambatana nayo.

"Ni hisia nzuri. Mtu anaweza kupanga mambo yake . Mtu hafanyi mambo kiholela, angalau unaweza kuwajibika. Unajua maana ya unachokifanya. Sio kama kitambo wakati mtu aliishi kama nyani, unachokipata ni chako tu" Alisema.

Mulamwah pia alifichua kwamba licha ya kuwa alitengana na  baby mama wake, bado huwa anapata nafasi ya kumuona bintiye mara kwa mara.

Alisema kuwa mpenzi wake wa zamani Carrol Sonnie hajamuwekea vikwazo vyovyote vya kumuona binti yao.