"Mapenzi yetu ni dira ya wenye wivu," Bilionea Grand P azungumzia mahusiano yake na Eudoxie Yao

Muhtasari

•Grand P amesisitiza kuwa ndoa yake na mwanasoshalaiti huyo kutoka Ivory Coast ni imara na ya kudumu.

•Wawili hao ambao huvutia ufuasi mkubwa kutokana na utofauti mkubwa wa kimaumbile kati yao wamekuwa kwenye mahusiano kwa kipindi cha takriban miaka miwili.

Image: INSTAGRAM// GRAND P

Mwanamuziki mashuhuri kutoka Guinea Moussa Sandiana Kaba almaarufu Grand P amethibitishia wakosoaji kuwa bado hajapoteza kipenzi chake Eudoxie Yao.

Wikendi hii bilionea huyo aliandamana na Bi Yao katika ziara yake nchini Gabon ambapo walipokewa na mashabiki wao kwa upendo mkubwa.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook Grand P amesisitiza kuwa ndoa yake na mwanasoshalaiti huyo kutoka Ivory Coast ni imara na ya kudumu.

"Wanandoa wa milele, upendo wetu ni dira ya wenye wivu" Grand P aliandika chini ya picha yake na mpenzi huyo wake.

Mwanamuziki huyo mwenye maumbile ya kipekee aliendelea kumsherehekea mpenziwe kwa jumbe tamu za mapenzi.

❤️❤️❤️🇬🇦🇬🇦

Posted by Grand P on Saturday, February 26, 2022

Haya yanajiri miezi michache baada ya  Eudoxie Yao kutangaza kuwa ametengana na bilionea huyo na kueleza kuwa ameamua kuangazia muziki wake tu baada ya kuchoka na mapenzi.

Licha ya tangazo hilo wapenzi hao wawili walionekana pamoja mara kwa mara ila hali ya mahusiano yao haikueleweka vizuri mpaka sasa wakati Grand P amedhihirisha wako poa kimapenzi.

Hivi majuzi Bi Yao ambaye ametunukiwa na makalio makubwa kweli alimtaja Grand P kama mpenzi wake wa zamani baada ya kumuona akijiburudisha na wanadada wengine kwenye bwawa la kuogelea.

Wawili hao ambao huvutia ufuasi mkubwa kutokana na tofauti kubwa za kimaumbile baina yao wamekuwa kwenye mahusiano kwa takriban miaka miwili.