Prof Wajackoyah aahidi kuachilia wafungwa wote wa bangi akichaguliwa kuwa rais

Muhtasari

•Mgombea urais huyo kwa tikiti ya Roots Party ameahidi kulinda watumizi wote wa mihadarati hiyo pindi atakaponyakua ushindi wa urais.

•Pia ameahidi kulinda haki za polisi huku akidai kuwa anafahamu changamoto zote ambazo huwa wanapitia kwa kuwa alikuwa mmoja wao.

Profesa George Wajackoyah
Profesa George Wajackoyah
Image: HISANI

Mgombea urais mwenye utata George Wajackoyah ameahidi kuwaachilia huru wafungwa wote walitiwa gerezani kwa sababu ya kupatikana na bangi iwapo atashinda kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti. 

Hivi majuzi alipokuwa anajipigia debe katika eneo la Magharibi, Wajackoyah alisema uvutaji bangi sio kosa kubwa linalostahili kupelekea kifungo cha jela.

Mgombea urais huyo kwa tikiti ya Roots Party ameahidi kulinda watumizi wote wa mihadarati hiyo pindi atakaponyakua ushindi wa urais.

"Wale watu ambao wamefungwa jela kwa kuvuta tundu la bangi, tarehe 9 mwezi wa nane wanatoka tu! Huwezi kuenda ukafunga jamii nzima, unachukua mtu ambaye amepatikana na katundu, dhamana inakuwa 20,000! Bibi yake, watoto wanaanza kuwa chokora. Alafu unasema sheria inafanya kazi," Wajackoyah alisema.

Wajackoyah alisema analenga kumaliza wizi nchini wakati wa utawala wake. Aliahidi kurejesha hukumu ya kifo kwa wote ambao watapatikana na kosa hilo.

"Nitatengeneza kamba ya kunyonga wezi. Nitaomba bunge wanipatie mamlaka hayo. Nikiwa Amri jeshi Mkuu, wale ambao wameiba watajitetea wakishindwa wanyongwe Uhuru Park," Alisema.

Wajackoyah pia aliahidi kulinda haki za polisi huku akidai kuwa anafahamu changamoto zote ambazo huwa wanapitia kwa kuwa alikuwa mmoja wao.