Mulamwah afunguka sababu zake kumvua nguo hadharani aliyekuwa mpenziwe, Carol Muthoni

Amesema hana majuto yoyote kufuatia madai aliyoibua hivi majuzi dhidi ya Muthoni

Muhtasari

• Mulamwah alisema alitafakari sana kabla ya kutengeneza video akimshtumu Muthoni kwa kujaribu kuavya mimba, kukosa uaminifu katika ndoa kati ya madai mengine.

•Alifichua kuwa aliafikia hatua ya kufunguka kufuatia uvumi mwingi ambao ulikuwa unaendelea kuhusu kilichowatenganisha.

Image: INSTAGRAM/CAROL SONNIE

Mchekeshaji mashuhuri David Oyando almaarufu Mulamwah amesema hana majuto yoyote kufuatia madai aliyoibua hivi majuzi dhidi ya mpenzi wake wa zamani mwigizaji Caroline Muthoni.

Akiwa kwenye mahojiano na Sauti TV, Mulamwah alisema alitafakari sana kabla ya kutengeneza video akimshtumu Muthoni kwa kujaribu kuavya mimba, kukosa uaminifu katika ndoa kati ya madai mengine.

Mulamwah alidai kuwa madai aliyoibua dhidi ya mpenzi huyo wake wa zamani ni baadhi tu ya maovu mengi aliyoyafanya walipokuwa kwenye mahusiano.

"Kabla nichapishe kitu huwa nachunguza mambo mengi kwanza. Sina majuto yoyote kwa yale niliyosema. Ndio maana nilikuwa nimesema hapo awali kuwa sifai kufunguka kwa kuwa hakuna jambo nzuri. Hiyo ni sampuli tu ya mambo mazuri ambayo naweza kusema, mengine hayasemeki," Mulamwah alisema.

Mchekeshaji huyo alifichua kuwa aliafikia hatua ya kufunguka kufuatia uvumi mwingi ambao ulikuwa unaendelea kuhusu kilichowatenganisha.

Alisema aligundua kuwa vuta nikuvute iliyokuwa inaendelea kati yake na Muthoni haikuwa ya manufaa yoyote kwao ndiposa akaamua kujitokeza kueleza yaliyotokea.

"Nilikaa tu chini nikaona hii kuvurutana haisaidii, hainitengenezei pesa wala kutengenezea Carol. Ilikuwa inanufaisha wanablogu tu ambao walikuwa wanaandika stori. Sina majuto yoyote kwa kuwa ni mimi nilichukua simu na nikarekodi. Kuna mengi sana," Alisema.

Baba huyo wa binti mmoja alitetea hatua yake ya kufunguka huku akidai kuwa alishinikizwa na mambo mengi kufanya uamuzi huo.

Muthoni alipotembelea studio zetu hivi majuzi alikataa kuzungumzia madai ambayo mpenzi huyo wake wa zamani aliibua dhidi yake.