TikTok yalemaza baadhi ya huduma zake Urusi

Muhtasari

• Kampuni ya mtandao wa kijamii ya TikTok imetangaza kulemaza kichupo cha utiririshaji wa moja kwa moja wa matukio nchini Urusi ili kama njia moja ya kuzuia kuenea kwa taarifa bandia. 

TikTok
Image: Facebook

Mtandao wa kijamii wa TikTok umetangaza kupunguza matumizi yake nchini Urusi kama njia moja ya kupiga vita propaganda na uvumi unaosambazwa kuhusu wanajeshi wa taifa hilo.

TikTok ambayo ni kampuni ya Uchina imesema haitositisha kabisa huduma zake Urusi basi wameamua tu kupunguza kwa kulemaza kichupo cha utiririshaji wa moja kwa moja yaani ‘livestreaming’ kama njia moja ya kujaribu kuleta marekebisho ya sheria kali dhidi ya utiririshaji wa moja kwa moja wa taarifa bandia na za uongo dhidi ya jeshi la Urusi.

“Katika mwanga wa sheria kuhusu taarifa bandia nchini Urusi, hatuna budi bali kusimamisha utiririshaji wa moja kwa moja wa matukio katika video za mtandao wetu ambapo tunaangazia athari za usalama za sheria hiyo,” TikTok waliandika katika Twitter.

Mashirika mbalimbali ya huduma za kila siku kama vile BBC, Netflix, Twitter na Meta ambayo inamiliki Facebook na Instagram miongoni mwa mengine yalitangaza kuondoa kabisa huduma zao nchini Urusi kutokana na kile walichokitaja kwamba taifa hilo limeivamia Ukraine kinyume cha sheria ya mizozo ya kimataifa.

Ila TikTok kutojiondoa kabisa kulitegemewa kwa sababu ni kampuni ya Uchina, taifa ambalo linazifagilia sana sera za Urusi na kutoipinga wala kuikashfu kwa kuvamia Ukraine.